22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kikwete rais bora wa mwaka 2015

kikweteNa Elias Msuya

GAZETI la Marekani la Sun Times na lenye umaarufu barani Afrika, limemtangaza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kama rais bora wa mwaka 2015 kwa Afrika.

Gazeti hilo pia limewataja watu wengine bora wa mwaka na kampuni bora yenye mchango kwa jamii.

Makundi ya tuzo yaliyokuwepo ni pamoja na mtu bora wa kimataifa wa mwaka, kiongozi bora wa Afrika, kampuni yenye mchango bora kwa jamii ya mwaka, mwanamajumuhi wa Afrika wa mwaka, mtu bora anayeishi uhamishoni, mtu mwenye ushawishi mwenye umri chini ya miaka 40 na balozi bora wa utalii kwa Afrika.

Katika makundi hayo, Rais Kikwete aliyeitawala Tanzania tangu mwaka 2005 hadi 2015, ametajwa kuwa kiongozi bora wa Afrika wa mwaka 2015.

“Rais Kikwete ameitumikia nchi yake kwa miaka 10 ya mihula miwili na ameshiriki moja kwa moja katika uteuzi wa mrithi wake, Rais John Magufuli hivyo kuendeleza utamaduni wa kidemokrasia wa kubadilishana madaraka, tofauti na nchi jirani na Tanzania ambazo viongozi wake wamekuwa wakivunja Katiba ili kuendeleza matamanio yao ya kisiasa,” limesema gazeti hilo.

“Rais Kikwete amepokea heshima nyingi kwa utendaji wake bora na shahada za udaktari wa heshima kutoka vyuo vikuu vingi. Afrika itaendelea kumhitaji kwa upatanishi wa amani alioufanya si alipokuwa tu rais, bali hata alipokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10.”

The African Sun Times ni gazeti kubwa zaidi la wiki nchini Marekani na limekuwa likichapishwa kwa miaka 37 iliyopita.

Mhariri wake mkuu Dk. Chika Onyeani ameshinda tuzo 73 za uzoefu katika uandishi wa habari na kujihusisha na utetezi wa haki za binadamu.

Dk. Onyeani pia ni mwandishi wa vitabu maarufu kama vile Capitalist Nigger: The Road to Success, Roar of the African Lion, The Broederbond Conspiracy (The Black James Bond) na kitabu cha watoto “ODUM: The Lion.”

Mbali na Rais Kikwete, tuzo ya mtu bora wa kimataifa wa mwaka 2015 imekwenda kwa Rais wa zamani wa Serikali ya Shirikisho la Nigeria, Goodluck Jonathan.

“Jonathan aliushtua ulimwengu baada ya kumwita Rais wa sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari na kukubali kushindwa uchaguzi wa Machi 29, 2015 na hivyo kusitisha hofu ya kutokea vurugu na umwagaji wa damu katika nchi hiyo huku akiahidi kutoruhusu damu za Wanaigeria kutumika katika matamanio yake kisiasa,” limeandika gazeti hilo.

Gazeti hilo limemsifu Jonathan kwa kujenga msingi wa demokrasia Afrika na kuwa dunia imeona ujasiri wake.
Kwa upande wa tuzo za kampuni bora inayotoa huduma kwa jamii kwa mwaka 2015, imekwenda kwa kampuni ya kimataifa ya Arik Air ya Nigeria.

“Ni kampuni pekee ya Afrika Magharibi iliyokidhi viwango vyote vya leseni vya mamlaka za usafiri wa anga za Marekani kupaa anga la Marekani. Chini ya meneja wake Robert Brunner, kampuni hiyo imeleta matokeo makubwa kwa kampuni nyingine katika kuwahudumia Wanigeria waishio Marekani.”

Kuhusu tuzo ya mwanamajumuhi wa Afrika bora wa mwaka 2015, imekwenda kwa Dk. Ron Daniels ambaye ni Rais wa Taasisi ya Black World and the Pan-African Unity Dialogue.

“Kuna mvurugano mkubwa ndani ya harakati za wanamajumuhi waishio uhamishoni, lakini Dk. Daniel amefanikiwa kuyaleta makundi yao pamoja na iwe ni Waafrika, Waafrika wa Marekani, Walatino na Caribbean. Dk. Daniel pia anakumbukwa kwa kazi yake ya miaka 20 kwa watu wa Haiti.

Katika tuzo ya mwanauhamishoni bora wa mwaka 2015, imekwenda kwa Balozi Dk. Erieka Bennett ambaye ni mwanzilishi na Rais wa Jukwaa la Waafrika wanaoishi uhamishoni (AU/DAF).

“Hakuna moyo wa kujitoa ambao Mwafrika aliye uhamishoni anaweza kuutoa kama kuacha starehe zake Marekani na kwenda Ghana kwa lengo la kujenga uhusiano kati ya Afrika na watu walioko uhamishoni,” limesema gazeti hilo.

Gazeti hilo limemwelezea Balozi Bennett kuwa alianzisha ubalozi Accra, Ghana na kutambuliwa na Serikali ya nchi hiyo.

Kuhusu tuzo ya mtu mwenye ushawishi zaidi na aliye na umri chini ya miaka 40, imekwenda kwa Linda Ikeji ambaye ni mwanzilishi wa blog ya lindaikeji.blogspot.com.

Gazeti hilo limesema Ikeji amefanikiwa kutoa ushawishi kupitia blog hiyo inayosomwa na mamilioni ya watu duniani kote.

“Akijulikana kama malkia wa blog ‘African Queen Blogger’ na gazeti hilo, Ikeji amewavutia wajasiriamali wengi wa Nigeria wanaume kwa wanawake huku akitoa misaada ya fedha na ushauri binafsi.”

Kuhusu balozi wa utalii wa mwaka 2015, tuzo hiyo imekwenda kwa Ikechi Uko ambaye ni mwanzilishi wa maonyesho ya Akwaaba Expo yanayofanyika kila mwaka nchini Nigeria na yanayowavutia watu kimataifa.

“Nenda popote Afrika na utaje jina la Ikechi, watu watamfahamu haraka na kusifu kazi zake za kukuza utalii wa Afrika.

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles