27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

KIKWETE AZINDUA TAASISI YAKE, MAJINA MAARUFU YA JMKF

Na CHRISTINA GAULUHANGA- DAR ES SALAAM


RAIS Mstaafu Jakaya Kikwete, amesema ana furaha baada ya kufanikiwa kuanzisha taasisi yake, huku ikiwa na majina ya watu wengi maarufu.

Taasisi hiyo iliyopewa jina la Jakaya Mrisho Kikwete (JKMF), ilizinduliwa Dar es Salaam jana sambamba na kufanya kikao cha kwanza cha bodi yake ya udhamini. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kikwete alisema tangu astaafu, hakuna siku iliyompa furaha inayofanana na uzinduzi huo.

“Hakuna siku inayofanana na hii kwangu baada ya kustaafu, ni imani yangu kuanzishwa kwa taasisi hii kutanisaidia kukamilisha maono, kiu na ndoto zangu katika maisha yangu hapa duniani,” alisema Kikwete.

Alisema wazo la uanzishwaji wa taasisi hiyo, alilipata kabla ya kustaafu, lakini alikuwa akipitia changamoto nyingi juu ya nini cha kufanya.

“Nilipata wazo la kuanzisha taasisi hii kabla sijastaafu, nilikuwa bado sijajua nifanye nini au sekta ipi. Nilipata mawazo mengi kutoka kwa rafiki zangu na ndugu na jamaa, wengi walinidokezea nianzishe mapema kabla watu hawajanisahau… nashukuru Mungu ndoto yangu imetimia,” alisema.

Alisema katika maisha yake yote tangu akiwa shule, alikuwa akitumikia jamii, hivyo ameona ni muda mwafaka kwake kujikita mbele ya jamii kutekeleza azma yake.

“Nimepata uzoefu, kujifunza mambo mengi nikiwa mtumishi wa Serikali. Napenda kuendelea kuitumikia jamii na katika maisha yangu naamini ushirikiano ndiyo jambo la busara, maana nimepata hata wadhamini kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema Kikwete.

Alisema malengo makuu ya taasisi yake, ni kushughulikia maendeleo ya jamii, afya, elimu kwa vijana na utawala bora.

Kikwete alisema taasisi yake imesajiliwa Februari 17, mwaka huu, ikiwa na wajumbe wa bodi ya udhamini tisa, wakiwamo viongozi wastaafu wa ndani na nje ya nchi, wanasheria, madaktari bingwa na wafanyabiashara wakubwa.

Aliwataja wajumbe wa bodi hiyo ni aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala.

 Wengine ni mwanasheria mzoefu, Balozi Mwanaidi Sinare ambaye alikuwa balozi wa Tanzania katika nchi za  Uingereza na Marekani na mtaalamu bingwa wa upasuaji na tiba ya moyo, Profesa William Mahalu, ambaye pia alikuwa Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando, Mwanza.

 Pia wamo Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Said Salim Bakhresa, Abubakar Bakhresa na mtaalamu wa masuala ya kibiashara ya kimataifa, Genevieve Sangudi ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mkuu wa Kanda ya Afrika Mashariki na Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu katika Ofisi ya Waziri Mkuu Malaysia, Dato Sri Jala ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Matokeo Makubwa sasa (Pamendu) nchini humo.

Kikwete aliwataja wengine kuwa ni Balozi wa zamani wa Marekani nchini, Charles Stith ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Marais wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Boston Jimbo la Massachusetts nchini Marekani na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Umoja wa Mataifa (Unitar), Dk. Carlos Lopes ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Siasa katika Ofisi ya Utendaji ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-moon.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles