Kikundi cha wizi wa mtandao kwenye mabenki chanaswa Rwanda

0
727

KIGALI, RWANDA

KIKUNDI cha  wadukuzi kinachowajumuisha raia kutoka mataifa ya Afrika Mashariki kimetiwa nguvuni nchini Rwanda kilipokuwa kikijaribu kuingilia mifumo ya benki.

Ofisi ya Taifa ya upelelezi nchini Rwanda imesema wadukuzi hao walipanga kuiba fedha kutoka kwenye akaunti ya mteja wa benki ya Equity, lakini haikusema ni lini jaribio hilo lilifanyika.

Ofisi hiyo imesema kuwa kikundi hicho kinawajumuisha Wakenya wanane, Wanyarwanda watatu na Mganda mmoja.

Benki ya Equity Bank ni moja ya benki kubwa katika kanda ya Afrika mashariki na kati ikiwa na matawi yake katika mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Sudan Kusini na Jamuhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Ofisi ya taifa ya upelelezi nchini Rwanda imesema kuwa awali kikundi hicho cha wadukuaji kilifanikiwa kuingilia mifumo ya benki hiyo katika nchi za Kenya na Uganda.

Mwanzoni mwa mwaka huu Mkurugenzi mkuu mtendaji wa Equity Bank James Mwangi alinukuliwa akisema kuwa benki hiyo ilikabiliwa na majaribio 14,000 ya udukuzi wa mifumo yake.

Udukuzi wa mifumo ya kampuni si suala geni Afrika Mashariki.

Mwezi Machi , 2017 mwanaume wa makamo alishtakiwa kwa tuhuma za kudukua mfumo wa kifedha wa Mamlaka ya Mapato ya Kenya (KRA).

Udukuzi huo ulidaiwa kusababisha mamlaka hiyo kupoteza jumla ya shilingi bilioni nne za Kenya (dola 39 milioni za Marekani).

Alex Mutunga Mutuku, ambaye alishtakiwa makosa ya kutekeleza ulaghai kwa kutumia mifumo ya kielektroniki, alikanusha mashtaka hayo alipofikishwa mahakamani.

Upande wa mashtaka ulidai Bw Mutuku alikuwa sehemu ya mtandao mkubwa wa watu waliokuwa wakiiba pesa kutoka kwa taasisi na makampuni makubwa nchini Kenya.

Alidaiwa kutekeleza makosa hayo kati ya Machi 2015 na Machi mwaka huu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here