AKIWA na umri wa miaka 23 kwa sasa, kijana Abbas Nur na wenzake watatu wanasota gerezani nchini Sudan wakisubiri siku ya hukumu ya kunyongwa hadi kufa.
Nur, Mudthar Al-Reeh, Fadl Al-Mawla na Ahmad Jibril ni vijana hao wanaoishi gerezani huku wakishukuru Mungu kila siku inapokwisha bila kusikia wakiitwa kwenye kitanzi.
Wanne hao waliingia kwenye giza zito hilo kwa nyakati na makosa tofauti lakini kinachowakutanisha hapa ni kwamba waliingia hatiani wakiwa na umri chini ya miaka 18. Hoja ni kwamba hawakustahili kunyongwa kwa kuwa walifanya makosa wakiwa wadogo.
Makala haya yanamuangazia Nur aliyeingia kwenye mkasa huo Agosti 27, 2013, baada ya kugombana na kijana mwezake na kisha kumpotezea maisha kwa kumchoma kisu.
Kwa mujibu wa baba yake, Nur alikorofishana na rafiki yake wakati wakicheza mpira wa miguu na kilichofuata ni tukio la kumuua.
Baada ya hapo, Nur ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 15, alishikiliwa na polisi mjini Rufaa, akapandishwa kizimbani Januari 7, 2014, kabla ya kushukiwa na hukumu ya kifo miezi michache baadaye.
Hata hivyo, mwanasheria wake, Taha Fadl Taha, alikosa vikali hukumu hiyo, akisema Nur alifanya kosa hilo akiwa mdogo, hivyo haikuwa sahihi kwa Mahakama ya Rufaa kutaka ahukumiwe kama mtu mzima.
Haikuwa mwanasheria pekee, bali hukumu ya Nur ilivuta hisia za wengi, wakiwamo wananchi walioandamana nje ya Mahakama kila ilipofika siku ya usikilizaji wa kesi.
Pia, taasisi mbalimbali za kupigania haki za binadamu zilipasa sauti kwa nyakati tofauti, zikitaka Nur aondoshewe adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa kuwa alikuwa mtoto wakati anatenda kosa.
Mwaka 2017, Nur akiwa gerezani kusubiri kifo, alimwita baba yake anayetajwa kwa jina la Mohammed. Katika mazungumzo yao, Nur alimwmabia mzee wake huyo, “Baba, mamlaka za hapa gerezani zimeanza mchakato wa siku yangu ya kunyongwa. Wameshanipima ukubwa wa shingo na uzito wangu.”
Ikiwa ni miaka saba sasa tangu walipohukumiwa, bado Nur na wenzake watatu wanasota gerezani wakisubiri hukumu hiyo inayotajwa kukiuka Sheria ya Watoto ya Sudan ya mwaka 2010.
“Nur aliniambia kwamba anatamani anyongwe hata leo hii, kuliko kuishi akiwaza siku hiyo,” anasema baba yake. “Kila nikizungumza naye, ananiambia ‘hii inaweza kuwa siku yangu ya mwisho baba’.”
Kwa ujumla wake, hukumu ya Nur ni mwendelezo wa namna Sudan inavyoendelea kukiukwa haki za watoto, licha ya kuwapo kwa ulinzi utokanao na Sheria ya Watoto ya mwaka 2010.
Ripoti ya Kamati ya Haki za Watoto ya mwaka 2010 ilionesha kuwa bado watoto wameendelea kushushiwa hukumu za kunyongwa hadi kufa katika nchi hiyo yenye watu milioni 43.
Takwimu za mwaka 2019 zinaonesha kuwa watoto takribani 100 walihukumiwa kifo lakini ni 20 tu walioachiwa, huku wengine wakisubiri siku ya kunyongwa hadi wapoteze uhai.