23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, May 21, 2022

Kigwangalla: Tusibweteke kusema corona imeisha

Na JANETH MUSHI-ARUSHA

WADAU wa utalii nchini wakiwemo watoa huduma wameagizwa kuendelea kuchukua tahadhari zilizotolewa na wataalamu wa afya kwa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona ili kuwalinda watalii.

Agizo hilo limetolewa jana jijini Arusha na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati wa utoaji wa tuzo za pili za Hifadhi za Taifa (Tanapa).

Tuzo hizo zilitolewa kwa washindi 33 walioshinda makundi mbalimbali ya wadau wa utalii, waliotoa mchango katika sekta hiyo kufanya vizuri hasa katika kipindi cha janga la corona.

Kigwangalla alisema kuwa ni muhimu wadau wa utalii wakiwemo watoa huduma kuendelea kuchukua tahadhari ili watalii pamoja na watumishi wao wasipate maambukizi pamoja na kuendelea kuvutia utalii zaidi nchini.

Alisema endapo kila mdau wa sekta hiyo atafuata kanuni na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, itaendelea kujenga uaminifu kwa nchi ndani na nje ya nchi.

“Corona imeleta athari katika sekta ya utalii nchini na duniani kote kutokana na vikwazo vya usafiri lengo likiwa ni kudhibiti maambukizi, hivyo imepunguza idadi ya watalii.

“Tusibweteke kusema corona imeisha, tuwe macho na wageni ili wasituletee ugonjwa, tujikinge na kuwakinga maana akija mmoja anao ataambukiza wenzake, tuzidi kuchukua tahadhari kwa faida ya afya zetu na biashara kwa nchi yetu.

“Hivi karibuni tumeona matumaini ya sekta ya afya, hadi sasa kuna mashirika makubwa matano ya ndege za kimataifa zimeanza safari zake na kuleta watalii hapa nchini,” alisema Kigwangalla.

Aidha alisema wizara inathamini mchango mkubwa unaotolewa na wadau wa sekta hiyo wakiwemo wa sekta binafsi ambao unasaidia ukuaji wa uchumi.

“Hata hivyo nashukuru kwa ushirikiano tulioupata kwa wadau wetu kwani utafiti unaonyesha tusingechukua jitihada za haraka mapema sekta ya utalii ingeathirika kwa asilimia 75, ajira, mapato kwa Serikali ingepungua zaidi ndiyo maana tulianza kufungua taratibu,” alisema Kigwangalla.

Alipongeza wadau wote waliopata tuzo hizo, ambazo washindi wa jumla  waliochanganya aina zote za utalii na kuingizia mapato Tanzania ni Leopard Tours (wa kwanza), Zara International (wa pili) na Ranger Safari (wa tatu).

Awali Kamishna wa Uhifadhi Tanapa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Allan Kijazi, alisema lengo la tuzo hizo ni kuthamini michango ya wadau katika kukuza na kuboresha sekta hiyo muhimu.

Alisema hiyo ni namna ya kuongeza morali kwa wadau wa utalii ili kuweza kuongeza watalii na mapato yatokanayo na sekta hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamani Tanapa, Jenerali mstaafu George Waitara, alisema ni muhimu kuilinda sekta ya utalii kwani ina mchango mkubwa katika pato la taifa ambapo huchangia asilimia 17 huku katika fedha za kigeni ikiwa ni zaidi ya asilimia 25.

Alisema wanapongeza juhudi za Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali kipindi cha janga la corona ambazo zimechangia kuendelea kuboresha na kulinda sekta hiyo na kuwa kila mdau amechangia katika hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
191,642FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles