29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kigwangalla: Sioni matokeo chanya upandaji miti

Na BENJAMIN MASESE -MWANZA

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla amesema haoni matokeo chanya ya siku ya upandaji miti milioni moja kila mwaka na ameshauri ni vema shughuli hiyo ifanywe na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Alisema amekuwa akizunguka nchi nzima wakati akitekeleza majukumu ya wizara yake, lakini  hajawahi kuoneshwa shamba la miti, msitu au pori lililotokana na upandaji miti milioni moja kila mwaka, hivyo ni dhahiri hakuna matokeo chanya.

Dk. Kigwangalla alitoa kauli hiyo jijini  hapa jana wakati akizindua bodi mpya ya TFS.

Alisema nguvu inayotumika kupanda miti hiyo milioni moja na maandalizi ya sherehe hizo, ni vema ikatumika kuwezesha wakala huo kwani tangu uanzishwe miaka tisa sasa umeonesha mafanikio makubwa sana.

“Mimi nimekuwa nikishangaa sana kila mwaka kumekuwapo na sherehe za upandaji miti milioni moja, lakini sijawahi kuona matokeo yake, nazunguka sana wakati natekeleza majukumu yangu, sijawahi kuonyeshwa shamba la kijiji au pori ambalo ni matokeo ya upandaji miti hiyo.

“Ni vizuri sasa shughuli ikaachwa ifanywe na TFS, nguvu ile iliyokuwa ikitumika katika sherehe hizo ikageuziwa kwa wakala kwani baada ya kupandwa wataisimamia tofauti na sasa inapandwa haihudumiwi na mwisho inakufa halafu mwaka mwingine tena mnapanda,” alisema.

Alisema ikiwa miti na vyanzo vya maji havitatunzwa, Tanzania itarudi katika giza kwa sababu inawekeza katika nishati ya maji ili kupata umeme, hivyo mazingira yakiharibiwa basi viwanda vitashindwa kujiendesha kwa kukosa umeme.

Alisema hivi sasa Watanzania wanakadiriwa kufikia milioni 52, baada ya miaka kati ya 7 hadi 10 watafikia milioni 100, vile vile baada ya miaka 100 mbeleni watafika milioni 240, sasa viongozi wa sasa tusipotunza misitu  kizazi kijacho kitapata shida sana.

Dk. Kigwangalla alisema Watanzania asilimia 70 wanategemea kilimo cha kujikimu na asilimia 99 wanasubiri mvua, na hadi sasa athari za uharibifu wa misitu ulioanza kufanyika miaka 11 iliyopita zimeanza kuonekan.

“Hatuoni chakula cha kutosha, ukame, vyanzo vya maji vimeharibika na mambo mengi ambayo kila mmoja anayaona kwa macho,” alisema.

Alisema yapo baadhi ya mataifa yamefikia kusafisha maji kwa matumizi kutokana na kuchafuliwa na sumu, pia zipo nchi zinagawana maji katika maziwa, bahari na mito, lakini Tanzania tumebarikiwa kuwa na vitu hivyo ambapo aliwataka viongozi wote na Watanzania kupambana kuvitunza.

Hata hivyo, Dk. Kigwangalla alisema Watanzania wanapaswa kuelewa tunakoelekea ni lazima sheria zibadilishwe ili kuweka kiwango cha ardhi ambacho mtu anapaswa kumiliki kama sehemu ya makazi, malisho na mashamba.

Alisema hali hiyo imetokena na ongezeko la kasi la watu ikizingatiwa ardhi haiongezeki huku akisisitiza kwamba wakulima waanze kilimo cha umwagiliaji na ufugaji wa kisasa ndani ya eneo wanalomiliki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles