23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kigwangalla ashawishi mabalozi kuhusu utalii, kuisha corona

Na waandishi wetu – Dar es Salaam

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, amesema Tanzania iko tayari kupokea watalii kutoka China, India na mataifa mengine ambayo yameruhusu raia wake kusafiri nje ya nchi zao.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa jana, Dk. Kigwangalla aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, Balozi wa India, Sanjiv Kohli na Balozi  wa Umoja wa Ulaya, Manfredo Fanti.

Alisema Tanzania imefungua anga na kuruhusu ndege za abiria za kimataifa kutua hali iliyochangia kufunguka kwa sekta ya utalii kutokana na kuwepo kwa utayari, mazingira salama na maandalizi mazuri ya kupokea na kuhudumia watalii watakaowasili nchini wakati huu wa janga la corona.

Dk. Kigwangalla alisema ameamua kukutana na kuzungumza na mabalozi hao kuwaelezea utayari wa Tanzania kupokea watalii na hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kufungua Sekta ya Utalii  wakati huu wa janga la corona.

Alisema ameamua kukutana na mabalozi hao kwa kuwa  nchi zao zinaleta watalii wengi Tanzania, pia wana nafasi kubwa ya ushawishi na uwezo wa kuwahamasisha  mawakala wa utalii, kampuni za huduma za utalii na raia wa nchi zao kufanya safari za kitalii nchini.

Aliwaeleza mabalozi hao kuwa Tanzania ilichukua hatua mbalimbali kukabiliana na janga la corona, ikiwemo uzingatiaji wa masharti na matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mamlaka za afya nchini kuwaelimisha wananchi na kuwasisitiza kuzingatia kanuni za afya zikiwemo za uvaaji wa barakoa, matumizi ya vitakasa mikono, unawaji wa mikono mara kwa mara na kuepuka misongamano hatarishi hali iliyochangia kuwepo kwa maambukizi madogo ya ugonjwa wa corona.

Dk. Kigwangalla alibainisha kuwa Tanzania haikuchukua hatua kali za kuwafungia watu majumbani (Lockdown) kama yalivyofanya mataifa mengine kutokana na uchumi na shughuli za wananchi wengi kutegemea kipato cha siku kujikimu kimaisha.

Aliwaeleza mabalozi hao kuwa tayari Tanzania imezindua mwongozo wa taifa wa uendeshaji wa huduma na biashara ya utalii ambao unalenga kulinda afya na usalama  wa wadau wote wanaojihusisha na biashara ya utalii katika kipindi hiki cha janga la corona.

Dk. Kigwangalla aliwaeleza pia mabalozi hao kuwa watalii wote wanaowasili Tanzania katika kipindi hiki cha janga la corona watakuwa salama kutokana na uwepo wa mwongozo  huo kwa kuwa unatoa usimamizi kwenye viwanja vya ndege, hoteli za kitalii, watoa huduma za utalii, upimaji wa afya za wahudumu na wageni wote wanaoingia nchini pamoja na kukusanya taarifa za wasafiri wote.

Aliwahakikishia mabalozi hao kuwa mifumo ya huduma za afya na dharula nchini Tanzania iko tayari  kuhudumia watalii watakaokuwa wakiwasili kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

Alibainisha kuwa Tanzania ina hospitali za kisasa, maabara za upimaji zenye vifaa vyote vya huduma za dharura katika maeneo tofauti tayari kuhudumia watalii na wageni watakaoonyesha dalili za kuwa na ugonjwa wa corona.

Pia, amewaomba mabalozi hao wapange muda wa kutembelea maeneo mbalimbali yanayotumika kupokea watalii yakiwemo ya viwanja vya ndege, hoteli za kitalii na hifadhi mbalimbali ili kujionea utayari wa Tanzania katika kuwahudumia watalii.

Kwa upande wao mabalozi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wamemshukuru Dk. Kigwangalla kwa  juhudi anazozifanya kuhamasisha na kutangaza utalii na kuelezea hatua zilizochukuliwa na Tanzania kuonyesha utayari wake wa  kupokea watalii.

Wameipongeza Serikali kwa juhudi kubwa za kulinda uhifadhi na kuahidi kutoa ushirikiano katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za uhifadhi.

Mabalozi hao wamefurahishwa na uwepo wa mwongozo wa taifa wa  uendeshaji wa shughuli za utalii Tanzania pamoja na kuridhishwa na hali ya utulivu iliyopo inayowafanya wananchi waendelee na shughuli zao  za kila siku.

Aidha, wameridhishwa na hatua za haraka zilizochukuliwa na Tanzania kufungua anga jambo lililowezesha mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa kuanza kurejesha safari za anga nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles