NA GUSTAPHU HAULE
-Kibaha
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, amemtaka Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Beatrice Byalugaba atumie timu ya wataalum kufuatilia huduma ya upasuaji katika vituo vya afya na hospitali mkoani humo ziwe katika viwango vinavyohitajika.
Pia ametoa miezi mitatu kwa mganga huyo kuhakikisha anasimamia marekebisho ya chumba cha upasuaji katika kituo hicho wananchi wanaotumia kituo hicho waweze kupata huduma bora.
Dk. Kigwangala alitoa kauli hiyo jana mjini Kibaha alipopokea vifaa tiba 831 vyenye thamani zaidi ya milioni 400 vilivyotolewa na Mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka (CCM).
Vifaa hivyo ni kwa ajili ya kuboresha huduma ya afya nchini hususan kwa vituo vya afya, zahanati na hospitali za Jimbo la Kibaha Mjini
Alisema kazi ya Mganga Mkuu ni kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za huduma ya afya katika mkoa wake hivyo ni jukumu lake kuhakikisha maagizo yote yanayotolewa na Serikali yanafanyiwa kazi kwa wakati.
“Nimepita katika chumba cha upasuaji katika kituo hiki cha afya lakini yapo marekebisho madogo yanahitaji kufanyiwa kazi hivyo Mganga Mkuu nakupa miezi mitatu ya kufanya maboresho katika theatre hii iweze kufikia viwango,” alisema Kigwangala.
Alisema marekebisho hayo yafanyike katika vituo vyote vya afya na hospitali za Mkoa wa Pwani kuepusha madhara kwa wagonjwa wanaofuata huduma hiyo na hata wahudumu ambao wamekuwa wakitoa huduma ya upasuaji katika maeneo yao.
Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka (CCM), alisema vifaa hivyo vina thamani zaidi ya Sh milioni 400 ambavyo vitagawiwa katika vituo vya afya na zahanati katika jimbo lake na hata mikoa mingine itakapobidi.
Koka alisema mchakato wa kuagiza vifaa hivyo ulianza mwaka 2011 kwa kutoa Sh milioni 12 kwa ajili ya kuwaleta wataalamu kutoka Marekani kupitia Kampuni ya Project Cure.
Wataalamu hao walifanya uchunguzi kujua mahitaji katika vituo vya afya, zahanati na hospitali.