NA MWANDISHI WETU, Dar es Salaam
KIJANA Juma Neti anayedaiwa kumweka rehani mdogo wake, Adamu Akida, kwa maharamia wa dawa za kulevya nchini Pakistan, ametoroka  nchini na kukimbilia Afrika  Kusini.
Taarifa za uhakika ambazo MTANZANIA inazo kutoka kwa mtu wa karibu wa Neti, zimeeleza kuwa alitoroka usiku wa Julai 19 mwaka huu kwa kutumia gari binafsi hadi  Kenya ambako alipanda ndege kwenda Afrika   Kusini.
Neti anadaiwa alitoroka nchini ikiwa ni siku moja kabla ya polisi na vyombo vingine vya usalama  kuvamia nyumbani kwake Kunduchi Ununio wilayani Kinondoni  Dar es Salaam juzi, kwa ajili ya kutaka kumkamata.
Chanzo hicho   kilisema polsi waliambulia patupu kwa vile  tayari Neti alikuwa ameondoka siku moja kabla.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Â kabla ya kutoroka, Neti alionekana akiwa na mshirika wake wa biashara (jina linahifadhiwa kwa sasa) ambaye humtambulisha kuwa ni ofisa masoko wa moja ya kampuni zake za ndani na nje ya Tanzania.
Inadaiwa pia kuwa  mshirika huyo    ndiye msambazaji hodari wa madawa ya kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Taarifa zinasema kwamba watu hao kwa pamoja waliweza kutoroka kwa kutumia gari ndogo kupitia mipaka isiyo rasmi kati ya Namanga na Horohoro na kuingia Kenya.
Baadaye waliingia Nairobi kwa kutumia gari  tofauti na walilotoka nalo Tanzania. Jijini Nairobi  walipanda ndege kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Mtoa taarifa huyo alieleza kuwa haikuweza kufahamika haraka ni ndege gani waliitumia kutoka Nairobi hadi Afrika Kusini.
Neti anadaiwa kumweka rehani Akida ambaye ni mtoto wa mama yake mdogo, nchini Pakistani, kwa gharama ya Dola za Marekani 700,000 (zaidi ya Sh bilioni 1.5) baada ya kuchukua madawa ya kulevya kutoka kwa maharamia wanaomshikilia Mtanzania huyo.
Taarifa zinaeleza kuwa polisi wamekuwa wakimtafuta Neti kwa mda mrefu bila mafanikio kwa tabia yake hiyo ya kujihusisha na biashara hiyo haramu.
Inaelezwa kwamba Neti amekuwa na utajiri wa kutisha ghafla na amekuwa miongoni mwa Watanzania wenye ukwasi mkubwa tofauti na miaka michache iliyopita ambako alikuwa mtu wa kipato cha kawaida.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, hivi karibuni Neti aliingia ubia na kampuni moja ya nchini China (jina halijafahamika) baada ya kuwekeza Dola za Marekani 400,000 (zaidi ya Sh milioni 800).
Katika mlolongo huo wa matukio kuna taarifa za kuwapo mtandao mkubwa unaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ambao huwapeleka vijana katika nchi zinazotengeneza dawa hizo na kuwaweka rehani.
Kwa mujibu wa  mtandao huo, vijana wengi hupoteza maisha kwa kuuawa na maharamia hao wakuu wa biashara hiyo ya ‘unga’ baada ya waliowaweka rehani kushindwa kupeleka fedha.