Kigogo TPRI akamatwa baada kesi ya ubakaji kuamriwa ianze upya

0
836
Mfanyakazi wa Taasisi ya kusimamia na kudhibiti Viuatilifu Tanzania (TPRI), Aristerico Silayo, akiwa chini ya ulinzi wa polisi kwa madai ya kumbaka mtoto wake baada ya kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana.

JANETH MUSHI-ARUSHA

KIGOGO anayefanya kazi katika Taasisi ya kusimamia na kudhibiti Viuatilifu Tanzania(TPRI),Aristerico Silayo, anayedaiwa kumbaka mtoto wake amekamatwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kuamuru shauri lililokuwa likimkabili lianze upya.

Mahakama hiyo jana ilipanga kutoa  hukumu katika rufaa ya  kesi ya mwanafunzi wa miaka 11 anayedaiwa kubakwa na baba yake mzazi (Silayo).

Rufaa  hiyo iliwasilishwa na upande wa Jamhuri Mahakama Kuu ya Tanzania,Kanda ya Arusha mbele ya Jaji Yohane Masara, baada ya kutokuridhishwa na hukumu iliyotolewa na Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi.

Rufaa hiyo iliyotokana na shauri namba 339,2017, ilisikilizwa katika mahakama hiyo ya chini katika kikao maalum baada ya mahakimu kupewa (extended jurisdiction),kusikiliza kesi za Rufaa zilizopangwa kusikilizwa na Mahakama Kuu, ili zitolewe uamuzi haraka.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aziza Temu jana Jamhuri iliwakilishwa na Wakili Mweteni Azael huku mtuhumiwa huyo akiwakilishwa na Wakili John Shirima.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Aziza alisema Mahakama hiyo inatupilia mbali mwenendo wa shauri hilo lililosikilizwa awali na kuamuru lianze kusikilizwa upya kwa Hakimu mwingine ili haki ipatikane kwa pande zote mbili na kuwa shauri hilo linapaswa kusikilziwa kwa haraka kwani limekaa mahakamani muda mrefu.

Alisema baada ya kupitia mwenendo wa shauri hilo, mahakama hiyo inajielekeza katika taratibu zilizotumika kuliendesha ambapo usikilizwaji wa awali ulikuwa kinyume na Sheria ya Ushahidi nchini iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006.

“Tukitazama mwenendo huo tunaona Hakimu alimuuliza mhanga maswali mengi ya kutaka kujiridhisha, nadhani alipaswa kuweka maswali machache na kumwongoza mtoto huyo kuahidi kusema ukweli.

“Hakimu alipuuzia marekebisho ya sheria hiyo ambayo yanasema mtoto mdogo anaweza kutoa ushahidi bila kuchukuliwa kiapo,”

“Kwa msingi wa sheria hiyo mahakama ya awali ilipaswa kumruhusu mhanga kusema ukweli mahakamani, hiyo ilisababisha kufifisha haki ya pande zote mbili,”alisema hakimu

“Mahakama hii inaona nafuu pekee inayoweza kupatikana na haki ionekane bado nashawishika ili haki ionekane imetendeka kuna haja ya shauri hili kuanza kusikilizwa upya kwa hakimu mwingine, natupilia mbali mwenendo wa shauri hili na mrufani arudi mahakama ya awali kesi ianze kusikilizwa,”aliongeza.

Awali kabla ya kusoma hukumu hiyo, hakimu huyo alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, Jamhuri walidai ushahidi wa mhanga, daktari aliyemfanyia uchunguzi pamoja na mwalimu aliyegundua mtoto huyo alikuwa akifanyiwa ukatili huo ulikuwa ukifanana na ulikuwa unatosheleza kumtia mjibu rufaa hatiani kwani ulikuwa wazi kuwa alikuwa akimwingilia binti yake.

Alisema katika mawasilisho wakili wa utetezi alidai kesi hiyo ni ya kutunga na ilikuwa akitengenezwa huku akidai kulikuwa na mkanganyiko wa baadhi mashahidi wa jamhuri.

Baada ya uamuzi huo mtuhumiwa huyo alikamatwa na jeshi la polisi na kupelekwa kituo cha kikuu cha polisi mkoani hapa ambapo katika rufaa hiyo jamhuri wanapinga hukumu iliyotolewa Desemba 14 mwaka jana katika shauri namba 339 la mwaka 2017 iliyotolewa na Hakimu Mkazi Gwantwa Mwankuga.

Awali Juni 27, mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk. Adelardus Kilangi, alisema ofisi yake inafuatilia sakata la mtoto huyo anayedaiwa kubakwa na baba yake mzazi, ambaye licha ya kubainika ana makosa aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here