27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

KIGOGO NASA ATAKA BAADHI YA MAENEO KENYA YAJITENGE

MSHAURI wa kiuchumi wa Muungano wa Upinzani nchini Kenya (NASA), David Ndii, ameibua mjadala mkali baada ya kusema katika mahojiano ya televisheni kuwa wakati umefika kwa sehemu nyingine za Kenya kujitenga.

Hilo limekuja baada ya mwanasafu huyo maarufu wa Gazeti la Saturday Nation kutupia waraka, ambao alisema alitumiwa na mmoja wa wasomaji wake ukichochea kujitenga na makabila mawili pekee yaliyotoa rais tangu Uhuru wan chi hiyo.

Waraka huo ulitoa wito kwa baadhi ya makabila ya Kenya kujitambua na kisha kujitoa kutoka kile alichokiita ‘makabila makuu’.

Sehemu ya waraka huo ulisomeka: Sisi watu wa Magharibi mwa Kenya, Luo, Luhya, Tsos, Kisii, Pwani ya Kenya, Kaskazini Magharibi mwa Kenya tumedhamiria kuwasilisha shauri kwa  Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu mjini Banjul, Gambia kutafuta haki yetu ya kuunda taifa letu lenyewe.

Mkataba wa Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu maarufu kama ‘Mkataba wa Banjul’ ni chombo cha kimataifa cha haki za binadamu kilicholenga kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi Afrika.

‘Niliutuma ujumbe ule katika mtandao wa jamii kwa sababu ni mimi niliyezua mjadala kupitia safu zangu kwa vile ulitumia lugha ninazotumia kama vile Kenya ni ‘ndoa katili’, alisema mshauri huyo wa uchumi wa NASA.

Akizungumza katika mahojiano ya televisheni juzi, Ndii aliulizwa na mtangazaji Larry Madowo iwapo anadhani maeneo yaliyogawanyika kwa kura baina ya NASA na Jubelee katika uchaguzi uliofanyika Jumanne wiki tatu zilizopita yanapaswa kutengana.

Dk. Ndii alijibu. “Watu wanazungumza hilo si mimi tu, picha utakayoiona katika mitandao ya jamii ndiyo hiyo ninayoizungumza,” alisema.

Aidha Dk. Ndii alionya Kenya inahitaji kubadilika katika siasa vinginevyo mabadiliko yasipokuja yatakuja kwa njia ya risasi.

Alisema iwapo haki yao haitapatikana mahakamani ambako mgombea urais wa NASA, Raila Odinga amefungua kesi kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, watatumia nguvu ya umma.

Alipoulizwa haoni iwapo hilo litasababisha vifo kama ilivyotokea baada ya uchaguzi wa 2007, Ndii alijibu kuwa yeye mwenyewe hajali hilo na yupo tayari kufa ilimradi tu mabadiliko yaje.

Dk. Ndii ni mmoja wa wanasafu wenye utata zaidi nchini Kenya, ambaye huzua mijadala katika masuala ya uchumi, siasa na utawala.

Amekosolewa kwa kauli yake hiyo na wakati huo huo kuungwa mkono na Wakenya, hali inayoonesha mpasuko mkubwa uliopo pande mbili.

Wakosoaji wake hasa kutoka Mlima Kenya, linakotoka moja ya makabila mawili yanayolalamikiwa na upinzani wametoa wito akamatwe kwa kutoa matamshi ya kichochezi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles