Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linaendelea kuwashikilia wafanyakazi wanane wa Kampuni ya Uda-Rapid Transit (UDART) akiwamo kigogo wa idara wa fedha ambao wanadaiwa kuhusika katika mtandao wa uhujumu wa mapato ya mabasi ya mwendokasi kwa kuchapisha tiketi feki kwa abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema kuwa watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa huku wengine 18 wakiachiwa kwa dhamana.
Alisema upelelezi utakapokamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kwa kosa la uhujumu uchumi.
“Bado tunawashikilia watuhumiwa wanane ambao walishiriki moja kwa moja tukio hilo huku wengine 18 ambao walishiriki kwa mbali tumewapa dhamana wakati tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Mambosasa.
Kamnada Mambosasa alisema, watuhumiwa hao wamefanyakosa hilo la uhujumu mradi wa Serikali ambao ni wa kitaifa na kimataifa kwa kutaka kufifisha jitihada za Serikali.
“Mradi huu unalitangaza Jiji la Dar es Salaam na taifa kwa ujumla kimataifa hivyo kwenda kinyume na jitihada hizo za serikali ni sawa na uhujumu uchumi, upelelezi unaendelea na watuhumiwa watafikishwa mahakamani haraka iwezekanavyo,” alisema Mambosasa.
Pamoja na hali hiyo alitoa tahadhari kwa Kampuni ya Udart, kuwa makini wakati wa kutoa ajira na kuwataka kufuata vigezo muhimu ili kuepuka kuajiri watu wasiokuwa na sifa.
Hivi karibuni MTANZANIA katika ripoti yake maalumu ya Juni mwaka huu, kuhusu usafiri wa mabasi hayo ilifichua namna wajanja wanavyotumia mwanya wa kutokusanya mapato kieletroniki na kusababisha hasara kwa serikali kukosa mapato yake stahiki.
Chanzo cha kuaminika kiliambia MTANZANIA kuwa kwa muda wa miezi miwili ilibanika kushuka kwa kasi kwa mapato Kituo cha Kimara kutoka makusanyo ya Sh milioni 20 hadi 25 kwa siku wakati yaliyokuwa yakikisanywa kupitia mfumo wa kieletroniki na kufikia hadi Sh milioni 10 kwa siku.
Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, walifanya uchunguzi na kubaini mtandao huo wa wizi huku mmoja wa kigogo wa juu wa kampuni hiyo naye alikamatwa na polisi.
Inadaiwa wafanyakazi hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa (majina yanahifadhiwa kwa sasa kwa sababu za kiuchunguzi), waliunda mtandao maalumu wa kufyatua tiketi feki na kujipatia mamilioni ya fedha.
Mradi huo wakati unaanza mwaka 2016, ulikuwa unabeba abiria 75,000 na kwa sasa idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia 200,000 na kwa kila safari hulazimika kulipa Sh 650 ukijumlisha kwa idadi hiyo mapato kwa siku yaliyokuwa yanakusanywa hufikia Sh milioni 130,000 ingawa kwa sasa yameshuka.
Katika mtandao huo imebainika mbali ya kufyatua tiketi feki pia wamekuwa wakifanya ujanja kwa kuwauzia watu wazima tiketi za wanafunzi ya Sh 200 badala ya Sh 650 huku kiwango kinachobaki kikingia katika mifuko ya wajanja.
Aprili 24 na Mei 16, mwaka huu makusanyo yalianza kuhujumiwa baada ya UDART kuingilia kati na kutaka kukusanya wao fedha huku wakipinga uwepo wa tiketi za Kiletroniki chini ya Kampuni ya Maxcom Afrika Plc.
Hatua hiyo iliifanya UDART kuingilia na kusimamia ukusanyaji wa mapato kupitia tiketi maalumu za mashine huku zikichanwa na wafanyakazi waliowekwa milango.
Awali mradi huo ulipoanza suala la makusanyo lilikuwa chini ya Kampuni ya Maxcom Africa ambao walikuwa wakikusanya Kieletroniki na udhibiti wa wizi huku UDART wakibaki na uendeshaji mabasi.