TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
ALIYEKUWA Katibu Kata wa Chama cha Wananchi (CUF) Kata ya Makurumla, Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam, Chahasi Shomari, amekihama chama hicho na kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Chahasi amerudisha kadi ya CUF na kukabidhiwa ya CCM jana na Katibu wa Siasa na Oganaizesheni wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Cholaje Mohamed, katika mafunzo ya viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya kata.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa kadi hiyo, Chahasi alisema amefanya uamuzi wa kuhamia CCM kutokana na haki walizokuwa wakizipigania akiwa CUF kuanza kutekelezwa na Rais Dk. John Magufuli pamoja na mshikamano uliopo ndani ya chama hicho tawala.
Alisema Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba, amekuwa akipigania haki za kiuchumi hasa kwa wafanyabiashara wadogo ambapo sasa wametambulika na Serikali.
“Kwa sasa machinga tumeanza kupata neema ya kutekeleza shughuli zetu bila kubughudhiwa na sasa tumepatiwa vitambulisho vya kutambua shughuli zetu,” alisema Chahasi.
Aliongoza kwamba, Mungu amemteua Rais Magufuli kuwakomboa wanyonge, hivyo Watanzania hawana budi kumuunga mkono.
Aidha, alilitaka kundi alilokuwa anafanya nalo kazi maarufu kama Mungiki, kuunga mkono uamuzi wake kwa kuwa siasa zinabadilika na kila mmoja anahitaji maisha bora, uchumi na maendeleo kwa Taifa.
Kwa upande wake, Cholaje alisema wanaamini Chahasi atakuwa na msaada mkubwa CCM kwa kuwa ataonesha mapungufu waliyonayo vyama vya upinzani kwa kusaidia kuyaeleza kwa wananchi.
“Ni siku ya neema kwa ngazi zote za chama kuanzia tawi hadi taifa kwa kuwa tumemchukua mpiganaji wa CUF ambaye alikuwa msaada mkubwa kwa Lipumba,” alisema Cholaje.
Aliongeza kuwa wanatarajia Chahasi atakuwa sehemu ya kampeni kuanzia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa.
Chahasi alikuwa mwanachama wa CUF tangu mwaka 1999 na anatajwa kuwa alikuwa ni sehemu ya wanamkakati wa waliofanikisha ushindi wa udiwani wa sasa kupitia CUF katika Kata ya Makurumla, Omari Kombo ‘Kijiko’.