Nyemo Malecela, Kagera
Aliyekuwa Meneja wa Chama cha Ushirika cha Ngara Farmers, Humphrey Kachecheba (50), amekutwa amefariki kwa kujiua kwenye nyumba ya wageni ya New Praise iliyopo Hamgembe Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Meneja huyo anadaiwa kujiua kutokana na kukabiliwa na msongo wa mawazo unaotokana na kufukuzwa kazi na kufunguliwa kesi mahakamani kwa upotevu Sh milioni 889, mali ya chama hicho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema meneja huyo wa zamani wa chama hicho cha Ushirika aligundulika ameshafariki Februari 3, mwaka huu saa tatu usiku akiwa chumba namba cha nyumba hiyo ya wageni.
Amesema uchunguzi wa awali wa Polisi, Kachecheba ambaye alikuwa mkazi wa Bunazi Kyaka alichukua chumba katika nyumba hiyo ya wageni tangu Januari 29 mwaka huu saa nne asubuhi akitokea Wilaya ya Ngara alikokuwa akifanyia kazi na aliendelea kuishi hapo hadi alipogundulika akiwa amefariki Februari 3 mwaka huu.
“Kwa muda wote inadaiwa alikuwa anashinda ndani ya chumba hicho amelala kila siku na kutoka saa mbili usiku na kurudi saa nne usiku.
“Chanzo halisi bado kinachunguzwa lakini hata hivyo kuna ushahidi mkubwa kuwa alijiua kwa sumu kutokana na msongo wa mawazo kufuatia kufukuzwa kazi na mwajiri wake jambo ambalo limethibitishwa na barua aliyokutwa nayo.
Mwili wa Kachecheba uligunduliwa na mhudumu na nyumba hiyo ya wageni, Odetha Edmund wakati alipotaka kufanya usafi ndani ya chumba hicho, baada ya kugonga mlango bila kupata majibu kutoka kwa mteja wake huku mlango ukiwa umefungwa kwa ndani.