30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kigamboni ilivyofanikisha ujenzi vituo vya afya

MWANDISHI WETU-DAR ES SALAM

MANISPAA ya Kigamboni ni kati ya halmashauri mpya hapa nchini iliyoanzishwa Novemba 6, 2015.

Hadi mwaka 2016 haikuwa na hospitali ya wilaya badala yake ilikuwa na Kituo cha Afya cha Vijibweni kilichopandishwa hadhi na kutumika kama hospitali  ya wilaya kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo ya jirani.

Desemba mwaka 2017 halmashauri ilipokea Sh milioni 400 kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ikiwa ni mpango wa maboresho ya vituo vya afya kote nchini na ujenzi ulianza Februari  2018 kwa kuwatumia mafundi wajenzi wadogo ambapo kila fundi alipewa jengo moja na kutakiwa kukamilisha kwa  mujibu wa mkataba walioingia na halmashauri.

Mfumo huu wa kuwatumia mafundi badala ya wakandarasi wakubwa (Force Account) kama ilivyozoeleka huko nyuma umeonesha mafanikio makubwa kwani majengo mengi yamejengwa na kukamilika kwa gharama ndogo tofauti na wakandarasi.

Mfumo huu ni shirikishi kwa kuwa wananchi wa eneo husika ni sehemu ya kamati za ujenzi kupitia kamati zao za afya na mitaa, wananchi hushiriki kuchangia nguvu zao  pamoja na ulizi wa mali kwa kipindi chote cha  ujenzi.

Katika Kituo cha Afya Kimbiji majengo yaliyojengwa na kukamilika ni wodi ya mama na mtoto, maabara, jengo la upasuaji, pamoja na jengo la kuhifadhia maiti.

Majengo hayo yamekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Kata za Kimbiji, Pembamnazi, Kisarawe II na wananchi kutoka Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani wanaoishi jirani na kituo hicho.

Hatua ya pili ni ufungaji wa vifaa ambapo baadhi ya maeneo vifaa vimeshakamilika na kuanza kutoa huduma kama maabara na wodi ya akina mama.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kigamboni, Dk. Charles Mkombachepa, anasema hadi kufikia Agosti mwaka huu vifaa vyote vyenye thamani ya Sh milioni 300 vitakuwa vimeshafungwa na kuanza kufanya kazi.

“Mara baada ya kuanza upanuzi wa kituo hiki jumla ya watumishi 32 wa kada mbalimbali za afya waliletwa na Serikali katika kuongeza ufanisi wa huduma,” anasema Dk. Mkombachepa.

KITUO CHA AFYA KIGAMBONI

Julai mwaka jana, halmashauri ilipokea tena Sh milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Afya Kigamboni ambacho kabla ya upanuzi kilikuwa na changamoto ya kuzidiwa na wagonjwa wengi.

“Wagonjwa kuwa wengi inachangiwa na mambo mengi, mojawapo ni ongezeko la watu, mfumo wa maisha lakini pia utoaji wa huduma bora katika kituo husika unaweza kuwavutia wananchi kufika na kuacha kwenda katika vituo vingine,” anasema Dk. Mkombachepa.

Naye Diwani wa Kata ya Kigamboni, Dotto Msawa, anasema kwa kipindi kirefu hata kabla ya kugawanywa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke kituo hicho kilikuwa na sifa ya huduma bora.

“Tunaishukuru Serikali kwa kutupatia fedha za upanuzi jambo ambalo kwa kushirikiana na wananchi na kamati za afya katika kata na wilaya tumeweza kusimamia ujenzi ndani ya miezi mitatu na kukamilisha majengo manne,” anasema Msawa.

Anasema ukamilishaji wa majejngo hayo upo katika hatua za mwisho za upakaji rangi na kisha kufunga vifaa ambavyo tayari vimeshaagizwa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

FORCE ACCOUNT

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni,Ng’wilabuzu Ludigija,anasema mfumo huo ni rahisi katika kutekeleza miradi kwa kutumia wataalam ambao haufuati taratibu za kikandarasi.

“Sisi tunanunua vifaa vyote vinavyohitajika na kumkabidhi fundi aliyeteuliwa, mfumo huu umepunguza gharama kwa karibu asilimia 50,” anasema Ludigija.

Mkurugenzi huyo anasema dhana kwamba kuwatumia mafundi wadogo ubora wa miradi hauzingatiwi ni potofu kwani kama halmashauri wanao wataalam wa ujenzi, wasanifu wa majengo na wakadiriaji wa majenzi  ambao ndiyo wasimamizi wa miradi hiyo kuanzia hatua ya awali kuhakikisha kilichopangwa kinafanyika na kukamilika kwa kiwango.

“Mafundi tunaowatumia ndio hao wenye makampuni makubwa ambapo kama tungetumia mtindo wa ukandarasi ni hawa hawa tungewapa kazi, tofauti ni kwamba kwenye ukandarasi angekabidhiwa sehemu ya ujenzi kisha yeye ananunua vifaa, kujenga na kisha kukabidhi jengo lililokamilika, mfumo ambao upo kisheria lakini ni wa gharama kubwa ukilinganisha na huu wa Force Account,” anasema.

HOSPITALI YA WILAYA

Katika mpango wa Serikali wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na hospitali ya wilaya, Halmashauri ya Kigamboni imetengewa Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi huo na tayari umeshaanza katika eneo la Gezaulole Kata ya Somangila karibu na yanapojengwa makao makuu ya wilaya na halmashauri hiyo.

Ujenzi wa hospitali hiyo pia unatumia mfumo wa Force Account na hadi sasa majengo saba yameanza kujengwa ambayo ni utawala, maabara, stoo ya dawa, jengo la mionzi pamoja na jengo maalumu la kufulia nguo za hospitali.

Mkurugenzi huyo anasema hadi kukamilika wanatarajia kutumia Sh bilioni saba na kwamba unatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa hekari 38.

Msimamizi wa mradi huo, Pius Mutechura, anasema kiwango hicho kinaweza kupungua kutokana na ushiriki wa wananchi na wadau wanaowasaidia vifaa kama kokoto, vifusi na mawe.

Mganga Mkuu, Dk. Mkombachepa anasema ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya una manufaa makubwa kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo ya jirani kwani kwa  sasa kuna baadhi ya huduma zinaposhindikana katika vituo vya afya na hospitali ya Vijibweni wanalazimika kuwapeleka Temeke au Muhimbili.

“Mara tutakapokamilisha ujenzi wa hospitali yetu huduma zote za msingi zitatolewa katika hospitali yetu ya wilaya,” anasema Dk. Mkombachepa.

Anatoa wito kwa wakazi wa Kigamboni kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara na hata kufika kupata ushauri wa kiafya katika zahanati, vituo vya afya na hospitali badala ya kusubiri hadi pale mtu anapozidiwa.

“Magonjwa mengi yanayowakabili wananchi kama kisukari, presha, uzito uliokithiri, utapiamlo na afya ya uzazi yanaweza kupunguzwa kwa kupata ushauri wa kitabibu bila hata kutumia dawa hivyo, nawaomba wananchi wajenge tabia ya kuwaona wataalamu wetu,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles