30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kifungo cha Ronaldinho kinatoa somo kwa mastaa

BADI MCHOMOLO 

BINADAMU anaishi mara moja tu, ukipata nafasi ya kuishi akikisha unaishi hadi mwisho wa maisha kwa kuwa nafasi hiyo haitokuja kutokea tena. 

Ronaldo de Assis Moreira, maarufu kwa jina la Ronaldinho Gaucho, alifanikiwa kuishi maisha ambayo alikuwa akiyaota kila siku kutokana na kutokea kwenye familia ya maisha ya chini. 

Alipata bahati ya dunia kumtambua kwenye mchezo wa soka, kwa watu ambao walianza kufuatilia soka miaka 2000, hauwezi kuliacha jina la Gaucho, aliufanya mchezo wa soka kuonekana kuwa kazi rahisi na aliongeza idadi kubwa ya mashabiki duniani. 

Kuanzia miaka ya 1957 hadi 1977, walilitaja jina la Edson Pele wa kule nchini Brazil, kuwa ni mmoja kati ya wachezaji bora kuwahi kutokea duniani, lakini Gaucho ameitikisa dunia vilivyo na watu kushindwa kumfananisha na mchezaji mwingine kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni. 

Aliufanya mpira kila atakavyo, mpira ulimpa heshima yake na dunia ikamuheshimu kutokana na kipaji chake, aliweza kutwaa mataji yote makubwa kwenye soka, hakuna taji kubwa ambalo aliliacha kama vile Kombe la Dunia, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Ligi Kuu Hispania, tuzo ya mchezaji bora wa dunia wa Ballon d’Or, lakini sasa yupo kifungoni. 

Ametufurahisha kwa kipindi kirefu, lakini sasa amebadilisha ubao na kutusikitisha kutokana na mwisho wake kuwa mbaya. 

Mchezaji huyo wa zamani wa Barcelona na AC Milan, mwenye umri wa miaka 40, aliwekwa ndani nchini Paraguay kwa siku 32 pamoja na kaka yake kutokana na kutumia pasi ya kusafiria ambayo sio sahihi. 

Tukio hilo lilitokea mapema Machi mwaka huu ambapo alikwenda kwa ajili ya kufanya matangazo wakati huo pasipoti yake ikiwa imezuiliwa nchini Brazil. Sababu ya kuzuiliwa kwa pasipoti hiyo ni kutokana na kushiriki kwenye uvuvi haramu, hivyo yeye na kaka yake wote paspoti zao zilizuiliwa. 

Kutokana na tamaa za kutaka kuyaweka sawa maisha yake, wawili hao waliamua kutengeneza paspoti feki za nchini Paraguay na kisha kuingia nchini humo kwa ajili ya kwenda kufanya biashara hiyo ya matangazo, wakakamatwa na kwenda jela. 

Hukumu yao ilikuwa inawataka kukaa jela kwa miezi sita, lakini wakaweza kukwepa kifungo hicho kwa kulipa dhamana ya pauni milioni 1.3, ikadaiwa kulipwa na nyota wa soka wa Barcelona, Lionel Messi, hivyo Gaucho na kaka yao wakaachiwa huru Aprili mwaka huu huku wakifanyiwa uchunguzi. 

Mbali na kuwa huru, lakini bado walikuwa chini ya ulinzi kwenye moja ya hoteli kubwa nchini humo ambayo inajulikana kwa jina la Capital Asuncion. 

Tangu hapo hadi sasa yupo chini ya uangalizi huku upelelezi ukiendelea. Wiki iliopita mahakama nchini humo ilikuwa inasikiliza rufaa yao, lakini ikatupiliwa nje jambo ambalo linawafanya kuendelea kuwa kwenye hoteli hiyo hadi sasa, lakini kama rufaa hiyo ingekubaliwa basi kuanzia jana wangekuwa huru. 

Hakuna kifungo ambacho unaweza kuwa huru hasa ukiwa chini ya uangalizi, Ronaldinho hana uhuru kwa kuwa yupo chini ya ulinzi kwenye hotel, hata kama anakula chakula ambacho anakitaka lakini bado anahitaji kuwa na familia yake, ndugu, jamaa na marafiki. 

Hana tofauti sana na wale ambao wamekuwa kwenye karantini kutokana na homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, lakini tofauti ya watu wa karantini ni kwamba wapo na familia zao nyumbani kwao, lakini sio kwa Ronaldinho ambaye hana nafasi ya kukutana na familia yake. 

Hii ina maana kuwa, hakuna mtu aliye juu ya sheria. Mwenye kukiuka sheria anachukuliwa hatua, hakuna ambaye alikuwa anafikiria Ronaldinho anaweza kusota hadi sasa kutokana na kile alichokifanya kwenye maisha yake ya soka. 

Hili ni somo kubwa kwa mastaa wa sasa ambao wanafanya vizuri kwenye idara zao na wanatikisha dunia huku wakiwa na majina makubwa, wanatakiwa kuendelea kuheshimu sheria za kila sehemu wakati huu wa ustaa wao na hata baada ya kumaliza kazi zao ambazo zinawapa majina makubwa

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles