25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

KIFUA KIKUU BADO TISHIO DUNIANI

Na HARRIETH MANDARI-DAR ES SALAAM


IFIKAPO Machi kila mwaka huwa ni mwezi wa kuadhimisha kifua kikuu (TB) duniani. Kilele chake huwa ni Machi 23.

Kifua kikuu ni ugonjwa unaowakabili watu wengi  duniani, hasa katika nchi zinazoendelea.

Ugonjwa huu husababishwa na bakteria anaejulikana kwa jina la Mycobacterium Tuberculosis, ingawa zipo jamii nyingine ya Mycobacterium zinazoweza pia kusababisha TB kwa binadamu. Pia husambaa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia hewa, wakati mgonjwa anapokohoa, kupiga chafya au mate yake yakiwa hewani.

Ni maradhi yanayoua zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa.
Dalili zake ni kuwa na kikohozi sugu, kukohoa damu, homa na joto kali, huku akitokwa na jasho jingi nyakati za usiku na kupungua uzito.


Njia mojawapo ya kumtambua mtu mwenye ugonjwa huu ni kumpima kwa kupiga picha ya X-ray kifuani, kupima kikohozi na damu ili kuchunguza vimelea mwilini.


Ili kuzuia kifua kikuu ni muhimu kwa mgonjwa kupimwa na ni kupewa chanjo.
Wataalalmu wa afya wanasema ipo haja ya kuendelea kutoa elimu juu ya ugonjwa huu kwa kuwa bado haufahamiki vizuri. Mratibu wa Uhamasishaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukimwi nchini,  Agatha  Mshanga anasema  Watanzania wengi hawana utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ikiwamo ugonjwa huu.

Anatoa mfano wa mwaka jana kwamba ni Watanzania 62,000 tu waligundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya kufika katika vituo vya afya.

Anasema Shirika la Afya Duniani (WHO), linataka angalau watu 160,000 wafike vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi. Hivyo hali inaonyesha kuwa kuna zaidi ya wagonjwa 98,000 ambao hawajafika kuchunguzwa,” anasema.

Anasema tatizo la Kifua Kikuu sugu nalo limekuwa changamoto kubwa kwa sekta ya afya nchini, ambapo hadi sasa kuna wagonjwa 2,000 waliogunduliwa.

“Tiba ya ugonjwa huu imeanzishwa rasmi ambayo ni ya muda mfupi kuanzia miezi tisa hadi 11, badala ya miezi 14-18 na  mgonjwa huanzishiwa tiba ndani ya saa 24 baada ya kugundulika,” anasema.

Naye Mratibu wa Kifua Kikuu migodini, Dk. Allam Tarimo anasema ili kutokomeza tatizo hili ni muhimu kwa Serikali kushirikiana na mashirika binafsi yanayojishughulisha na masuala ya magonjwa ikiwamo TB.

Anaasema hapa nchini vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma ya tiba ya ugonjwa huu bado havikidhi mahitaji ambapo kati ya vituo 1,400 ni asilimia 25 tu ya idadi hiyo ndiyo inatoa tiba hiyo.

Kwa upande wa hali ya ugonjwa huo kwa wafanyakazi wa migodini, anasema upo mradi maalumu ambapo wachimbaji hupatiwa huduma ya kupima mara kwa mara iwapo wamepata ugonjwa huo katika sehemu zao za kazi.

Anasema wafanyakazi hupimwa kwenye vituo ambavyo vimejengwa katika maeneno yenye migodi nchini na magonjwa mengine ikiwamo Ukimwi.

“Kama tunavyofahamu wachimbaji wengi wadogo wadogo hawana vifaa vya kisasa vya kujikinga na vumbi hivyo huwa rahisi kupata ugonjwa huo,” anasema.

Baadhi ya vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma hiyo nchini ni pamoja na Hospitali Maalumu ya Taifa ya Kutibu Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong’oto, kituo cha Palestina na Bugando. Miaka ya nyuma huduma hiyo ilipatikana katika Hospitali ya Kibong’oto pekee.

“Asilimia 13 ya waliogundulika kuwa na vimelea vya bakteria wa TB walitoka katika hospitali za binafsi ambao ni sawa na wagonjwa 65, kwahiyo, Serikali inapokuwa na ushirikiano na vituo binafsi inasaidia zaidi kutoa tiba kwa urahisi na kupata takwimu sahihi za wagonjwa hao kila mwaka,” anasema Dk. Tarimo.

Anaongeza kuwa wanashirikiana na wenye maduka ya dawa binafsi kutoa huduma hii, ambapo kupitia mradi wa kutokomeza TB nchini chini ya udhamini wa Mfuko wa Shirika la Kimataifa la Global Fund, tayari  kumefanyika mafunzo kwenye maduka 30.

Mmoja wa  wagonjwa wa Kifua Kikuu (jina tunalo) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam, anasema hakugundua kama anaumwa hadi alipofikia hali mbaya kutokana na kutojua dalili za ugonjwa huo.

“Nilianza kukohoa mfululizo nikaanza kunywa antibiotics lakini sikupona, nikaenda kwenye zahanati moja pale kwetu ya binafsi ambapo waliponipima walisema nina ugonjwa wa Typhoid na kunianzishia dawa ambazo nilizinywa hadi kuzimaliza bila kupona,” anasema.

Anasema baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio, hali ilizidi kuwa mbaya ndipo ndugu zake walipompeleka  katika  Hospitali ya Mwananyamala na vipimo vikaonyesha kuwa ana Kifua Kikuu, akaanzishiwa dozi katika kituo cha afya cha Palestina.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kibong’oto, Dk.  Riziki Kisonga wakati wa ufunguzi wa bodi ya hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka jana alisema baada ya kubaini ongezeko la TB katika mazingira hatarishi hasa katika mgodi wa uchimbaji madini ya Tanzanite  wa  Mererani, Hospitali ilianzisha huduma za vikoba kwa kutumia idara ya Afya ya Jamii kuelimisha wachimbaji wadogo wadogo.

“Mpaka sasa wachimbaji wadogo wadogo zaidi ya 2,000 wamechunguzwa  afya zao kati yao asilimia 4.5 wamekutwa na maambukizi ya TB na walipatiwa matibabu.

 

Takwimu
Hadi mwaka jana hapa nchini ilikadiriwa kuwa watu 120,000 wanaugua ugonjwa huu.

Taarifa ya Shirika la Msaada la Marekani (USAID), linasema kuwa mwaka 2007, vifo vilivyotokana na ugonjwa huu nchini vilikuwa 32,000.
Kwa mujibu wa WHO, dunia nzima mwaka 2012 watu milioni 8.6 waliambukizwa Kifua Kikuu na watu milioni 1.3 kati yao walifariki, wengi kutoka katika nchi zinazoendelea.


Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha mwaka jana, Tanzania ilikuwa nchi ya 15 kati ya 22 ambazo zimeathiriwa zaidi na ugonjwa huo. Mwaka 2012, watu milioni 8.6 waliambukizwa na kati yao milioni 1.3 walifariki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles