31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kifo ha Chadwick Boseman chastua mashabiki wa filamu

IMAN MKETEMA Na MASHIRIKA YA HABARI

TAARIFA za kifo cha Staa wa filamu ya hivi karibuni ya ‘The Black Panther’ Chadwick Boseman zimeshtua dunia hasa mashabiki wa filamu.

Wengi hawakuwahi kufahamu hadi mauti yalipomkuta jana iwapo Boseman mwenye miaka 43 alikuwa akisumbuliwa na kansa ya utumbo kwa miaka minne, kutokana na kulifanya jambo hilo siri.

Watu wanaomfahamu wanasema; Boseman ambaye alikuwa mkristu na wakati fulani kuwa sehemu ya kwaya ya vijana kanisani akiendelea kuishika imani yake hiyo alikuwa mwangalifu kwenye matumizi ya chakula na alikuwa anakula mbogamboga tu  ‘vegitarian’. 

Staa wa filamu ya ‘Captain America’ Chris Evans  ameandika ” Ni mtikisiko” na kwamba  Boseman “ameacha kazi nyingi za kushangaza ambazo ilibidi azifanye “.

Mastaa wa Hollywood, Chris Hemsworth na  Denzel Washington wametuma salamu za rambirambi wakieleza kushtushwa na kifo cha staa huyo wa  ‘Black Panther’ Boseman.

Taarifa iliyotumwa na familia yake imeeleza kuwa Boseman aliaga dunia akiwa nyumbani kwake Los Angeles  pembeni ya familia yake na mkewe ambaye ni mwanamuziki Taylor Simone Ledward aliyefunga naye ndoa mwaka 2019.

Boseman amezaliwa na kukulia Anderson, South Carolina, na ni Mmarekani mwenye asili ya Afrika.

Kwa mujibu wa yeye mwenyewe, kipimo cha  vinasaba (DNA)  kilionyesha kuwa mababu zake ni watu Krio kutoka  Sierra Leone, Yoruba kutoka Nigeria na Limba kutoka Sierra Leone.

Kabla ya kujipatia umaarufu mkubwa kupitia filamu ya ‘ The Black Panther’ aliyocheza pamoja na Lupita Nyong’o staa wa Hollywood kutoka nchini Kenya, Boseman amecheza filamu nyingine nyingi.

Lakini ni filamu hiyo ndiyo iliyoleta mapinduzi makubwa kwenye mauzo ya ambayo hadi sasa imeingiza 

Dola za Marekani bilioni 1.334, zaidi ikijizolea tuzo nyingi.

Boseman amefariki dunia wakati sehemu ya pili ya ‘The Black Panther’ ikitarajiwa kutoka ifikapo Mei 6,  2022.

Mbali na ‘The Black Panther’ Boseman ni mwigizaji aliyecheza filamu za kihistoria kama ‘The Express: The Ernie Davis Story (2008), 42 (2013), Get on up (2013), Marshall (2017), Da 5 Bloods (2020).

Kama ulikuwa unafuatilia sio tu kama aliigiza bali yeye ndio alikua mhusika mkuu wa filamu hizo ambazo ni matukio ya kweli yaliyotokea kipindi cha nyuma.

Kwa mfano kwenye filamu ya Get On Up, Boseman aliigiza kwa kuvaa uhusika wa mwanamuziki nguli wa soul marehemu, James Brown na akafanikiwa kuuvaa uhusika vizuri sana hadi akazawadiwa tuzo ya mwigizaji bora kwenye tuzo za NAACP huko nchini Marekani. 

Booseman ataendelea kubaki kwenye mioyo ya watu kama mwigizaji wa kuigwa wa karne ya 21 kutokana na staili na ubunifu aliokuwa akiutumia katika uigizaji wake.

MAISHA YAKE 

Chadwick Boseman alizaliwa Novemba 29,1976 South Carolina nchini Marekani.

Mama yake alikuwa muuguzi na baba yake alifanya kazi katika kiwanda cha nguo, akisimamia pia biashara ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sofa. 

Boseman alihitimu masomo ya juu ya sekondari kutoka shule ya T. L. Hanna mwaka 1995.

Akiwa shule msingi, aliandika mchezo wake wa kwanza, Crossroads, na kuigiza shuleni baada ya mwanafunzi mwenzake kupigwa risasi na kuuawa.

Boseman alikuwa ni mmoja wa mwanafunzi waliosoma  Chuo Kikuu cha Howard huko Washington, D.C., akihitimu mwaka 2000 shahada ya Sanaa.

Mwalimu wake alikuwa Phylicia Rashad, ambaye alikuwa mshauri wake pia.

Mwalimu wae huyo ndiye aliyesaidia kukusanya fedha ili Boseman na wanafunzi wenzake waweze kuhudhuria Programu ya Oxford Mid-Summer ya Chuo cha Maigizo cha Britten huko London, ambacho walikuwa wamekubaliwa. 

Boseman alitaka kuandika na kuelekeza (Writer& Director), na mwanzoni alianza kusoma uigizaji ili kujifunza jinsi ya kuhusika na watendaji. 

Baada ya kurudi Marekani alihitimu kutoka Chuo cha Filamu cha New York City. 

Boseman aliishi Brooklyn mwanzoni mwa taaluma yake. Alifanya kazi kama mkufunzi wa mchezo ya kuigiza katika Schomburg Junior, New York, Marekani. 

SAFARI YAKE YA UIGIZAJI

Boseman alionekana mara ya kwanza kwenye runinga mwaka 2003, katika kipindi cha ‘Watch’ mwaka huo huo, alicheza uhusika wa Reggie Montgomery katika michezo ya watoto.

Lakini alifukuzwa na uhusika huo kuchukuliwa na  nyota mwenza wa Black Panther, Michael B. Jordan.

Aliendelea  na kazi yake ya uigizaji kwenye tamthilia za Lawand Order, CSI: NY pamoja na ER huku akiandika maigizo mbalimbali.

Kazi yake ya Deep Azure iliyotumbuizwa katika Kampuni ya Congo Theatre huko Chicago baadae iliingia kwenye kinyang’anyiro cha Tuzo za Joseph Jefferson mwaka 2006.

Boseman aliigiza filamu yake ya kwanza ya The Express: The Ernie Davis Story. 

KUJULIKANA NA MWANZO WA MAFANIKIO

Mwaka 2013 filamu ya 42 ilitokana Boseman akiwa mhusika mkuu wa filamu hiyo. 

Filamu ambayo ilihusu maisha ya Jackie Robinson, mchezaji wa kwanza mweusi kucheza ligi kuu ya mchezo wa baseball huko nchini Marekani.

Boseman alikuwa akose nafasi hiyo ya kuigiza na kulikuwa kuna waigizaji wengine 25 na alikua aache kuigiza lakini alipata nafasi hiyo baada ya kujaribu tena kwa mara ya pili na kumfungilia njia kwani mwaka uliofuata aliigiza filamu nyingine ya maisha halisi ya mwanamuziki nguli wa soul marehemu, James Brown. 

Baada ya hapo umaarufu wake ukaanza kupanda kupitia kazi yake ya uigizaji mzuri na hivyo kupata kazi nyingine za filamu ikiwamo filamu ya ‘Gods of Egypt’.

MWANZO WA BLACK PANTHER

Mwaka  2016 Boseman alionekana kwenye filamu ya kampuni kubwa ya filamu duniani, Marvel ambayo filamu yao ya Avengers: End game ndio filamu inayoongoza kwa mauzo duniani baada ya moto wa Black Panther.

Mwanzoni alionekana kwenye filamu ya Captain America: Civil War akautambulisha uhusika huo kupitia Black Panther kwani ulikua kwenye vitabu vilivyoandikwa na marehemu Stan Lee. 

Lakini Boseman akiwa sambamba na Lupita alicheza vizuri na kuufanya uhusika huo wa Black Panther kuwa hai.

WAAFRIKA NA BLACK PANTHER

Filamu ya Black Panther ilileta msisimuko, kilichoonekana kuwafurahisha wengi ni utamaduni wa Waafrika na Wamarekani weusi kwa ujumla.

Filamu hiyo imeleta mapinduzi makubwa kwenye tasnia ya filamu duniani kwani ilipokelewa vizuri ulimwenguni kote.

Lakini hakuishia hapo ndani ya mwaka huo huo mwishoni Marvel waliachia filamu ya Avengers: Infinity War  na Boseman akiwemo tena akiuvaa uhusika wake ule ule wa Black Panther.

Avengers ilitokana na kuvunja rekodi ya mauzo ya Black Panther. 

Mwaka 2019 ukawa ndio mwaka wa mapinduzi kwani Marvel waliachia filamu nyingine Avengers: End game ambayo pia Boseman yupo akivaa tena uhusika wake ule ule wa Black Panther.

Maajabu hayakuishia hapo kwani filamu hiyo ilipiku mauzo ya filmu zote na kuwa filamu inayoongoza kwa mauzo ikiipita Avatar na Titanin.

FILAMU ZAKE ZA MWISHO

Katika mwaka huo huo wa 2019 Boseman aliigiza katika filamu ya kusisimua  ya Bridges 21 inayohusisha mambo ya mpelelezi wa NYPD ambaye alifunga madaraja 21 ya Manhattan ili kupata wauaji wawili walioua polisi.

Mwaka wa 2019, ilitangazwa kuwa Boseman ataonekana katika filamu ya kivita ya  Netflix ya Da 5 blood, iliyoongozwana Spike Lee. Filamu hiyo ilitolewa Juni 12, mwaka huu, miezi miwili kabla ya mauti kumkuta jana.

KIFO CHAKE

Boseman alisumbuliwa na saratani ya utumbo ya hatua ya tatu  mwaka 2016, ambayo mwishowe ilisonga hadi hatua ya nne kabla ya mwaka 2020. 

Hakuwahi kuzungumza hadharani juu ya kusumbuliwa na ugonjwa huo. 

Wakati wa matibabu aliendelea kufanya kazi na kukamilisha utengenezaji wa filamu kadhaa, kuanzia filamu ya Marshall (2017) hadi Da 5 Bloods (2020) na Ma Rainey’s Black Bottom na nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles