KIFO CHA BODABODA CHAZUA TAHARUKI SHINYANGA

0
517
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne

 

 

Na KADAMA MALUNDE-SHINYANGA

JESHI la polisi mkoani Shinyanga limelazimika kupiga mabomu ya machozi ili kuwatawanya waendesha pikipiki (bodaboda) waliokuwa wakiandamana kupinga kifo cha mwenzao anayedaiwa kuuawa na askari polisi aliyetajwa kwa jina moja la Edmund.

Tukio hilo lililosababisha shughuli za kijamii kusimama mjini hapa lilitokea jana muda wa saa moja asubuhi hadi saa sita mchana, ambapo kulizuka tafrani kubwa na kusababisha majibizano baina ya bodaboda hao kuamua kujibu mapigo ya polisi kwa kurusha mawe.

Hali hiyo imekuja siku moja baada ya bodaboda hao kulazimika kuwapiga mawe askari polisi kwa madai ya kusababisha kifo cha mwenzao,  Joel Gabriel Mamla (26) aliyefikwa na umauti baada ya kuanguka na kupasuka kichwa akiwa kwenye pikipiki aliyokuwa amebebwa na askari aliyemkamata.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Muliro Jumanne, alisema maandamano hayo si halali na wameamua kuyazuia kwa sababu yanahatarisha hali ya usalama na amani kwa kuwa hayajafuata taratibu.

Jeshi la polisi lililazimika kwenda msibani nyumbani kwa marehemu Joel na kuwatawanya waombolezaji kwa kuwakamata bodaboda hao na pikipiki zao na kusababisha vuta ni kuvute msibani hapo.

Mmoja wa bodaboda waliokuwa wanaandamana, Simoni Bundala, alisema wameamua kuandamana kwa madai ya kufikisha ujumbe serikalini kuwa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawaonea.

Tukio la kupoteza maisha kwa bodaboda huyo limetokea juzi saa 6.45 mchana katika eneo la Kona ya Buhangija barabara kuu ya Mwanza-Tabora.

“Wamekuja wanavutana kwenye pikipiki, walipofika eneo ambako yanatokea mabasi, askari akawa anaburuza miguu chini, mara akamkaba mwendesha bodaboda ili pikipiki isimame.

“Askari akamkaba roba dereva, ikabidi aachie usukani, alivyotaka kuruka akakuta pikipiki imeshahama barabarani ndiyo akakutana na alama ya barabarani akaibamiza, akaangukia jiwe,” alisema mmoja wa mashuhuda hao.

Shuhuda mwingine, Yahaya Kisewene, alisema walipoanguka chini ndipo bodaboda huyo akapiga kichwa kwenye jiwe na kuanza kuvuja damu puani na maskioni na kusababisha kifo chake hali iliyosababisha wananchi kuanza kumpiga askari.

“Wakati kichapo kikiendelea mtu huyo alipojitambulisha kuwa ni polisi lakini haikuwa rahisi wananchi kumtambua kwa sababu alivalia kiraia wananchi walidhani ni jambazi lilikuwa likitaka kumpora marehemu pikipiki.

“Licha ya utetezi huo wananchi hawakujali waliendelea kumshambulia na alifanikiwa kuwaponyoka na kukimbilia mji jirani kuokoa maisha yake,” alisema Kisewene.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Muliro alisema askari mwenye cheo cha CPL wa kikosi cha usalama barabarani na wenzake wawili walikuwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya ukamataji wa kawaida waendesha pikipiki wasiotii sheria za barabarani,

Alisema waliikamata pikipiki yenye namba za usajili MC 700 AWH SANLG iliyokuwa ikiendeshwa na Joel Gabriel Mamla kwa kosa la kutovaa kofia ngumu (helmet).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here