25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Kidunda Vs Katompa pambano la kufunga mwaka kesho

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

ZINAHESABIKA saa kabla ya pambano kubwa la kuwania mkanda wa WBF linalowakutanisha wakali wa ndondi Mtanzania Selemani Kidunda (JWTZ) na bondia kutoka DR Congo Tshimanga Katompa litakalopigwa kesho kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Mabondia hao pamoja na wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo iliyopewa jina la Usiku wa Mabingwa,wamepima uzito leo katika ukumbi huo, huku kila mmoja akiahidi kuchapa vibaya mwenzake.

Akizungumza baada ya kupima uzito, Kidunda amesema hana maneno mengi bali anawaahisi Watanzania kubakiza mkanda huo nyumbani ikiwa ni pamoja na kumlipia kisasi Mtanzania mwenzani Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ ambaye alipigwa na Katompa Oktoba mwaka huu.

Bondia George Bonabucha anayezichapa na Hassan Millanzi wa Zimbabwe, akipima uzito leo Desemba 25,2021 kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

“Mimi nimejiandaa vizuri Watanzania wasiwe na wasiwasi mimi mwenyewe najijua, nahisi watakachokiona ni tofauti na wanavyofikiria. Wasifananishe chumzi na sukari.

“Nawaomba tu Watanzania wajitokeze kwa wingi kesho, nitampa kile kilichomleta Tanzania. Napenda sana kufanya vitendo kuliko kuongea,” ametamba Kidunda.

Kwa upande wake Katompa pamoja na kumtupia dongo Kidunda,amemshukuru Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa mapokezi mazuri ya Watanzania aliyoyapata kupitia mchezo wa ngumi, akiamini hali hiyo itakwenda kuimarisha umoja na mshikamano wa nchi za Kiafrika.

“Kwanza namheshimu sana Rais wa Tanzania kwa mapokezi niliyoyapata. Jambo moja nilikija nalo hapa ni kuiwakilisha nchi yangu na Rais wangu wa Congo, amenituma kuja hapa nasikia kuna mwanajeshi kapotea njia, nimekuja kumtafuta na kumrudisha kambini,” amejitamba Katompa ambaye kitaaluma ni Mwanasheria.

Grace Mwakamele (kushoto) na Ruth Chasale wakitunishiana misuli baada ya kupima uzito leo Desemba 25,2021 kwenye ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Naye mratibu wa pambano hilo, Kapteni Selemani Semunyu, amewaahidi Watanzania burudani ya kutosha na ulinzi, hivyo kuwataka wajitokeze kwa wingi kuwasapoti mabondia watakaopeperusha bendera ya Tanzania.

Aidha mwakili wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa Duniani (WBF), Chacha Michael, amesema wamejipanga kusimamia pambano hilo kuhakikisha hakuna upendeleo wowote.

Jumla ya mapambano 13 yatapigwa kesho, kati ya hayo manne yatakuwa ya ubingwa wa PST ambayo yatawakutanisha ni Ismail Gariatano(Tanzania) dhidi ya Denis Mwale (Malawi), George Bonabucha(Tanzania) na Hassan Milanzi (Zimbabwe),Grace Mwakamele (Tanzania)na Ruthi Chisale(Malawi), Paul Magensta na Oscar Richard.

Ibrahim Class ambaye mpinzani wake kutoka Malawi ameshindwa kutokea atacheza na Kelvi Majiba pambano lisilo la ubingwa, wengine ni Vigulo Shafii na Ally Kilongola,Hamis Kibodi dhidi ya Idd Jumanne, Pascal Manyota na Joseph Mchapeni,Daniel Matefu na Haruna Swanga, Najma Isike atamkabili Leila Yazidu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles