MTANGAZAJI na mtayarishaji wa muziki nchini kupitia studio ya Tetemesha records, Sandu George ‘Kidbwoy’, amesema endapo wasanii wanataka kuwa na mafanikio katika kazi zao lazima wawe wabunifu.
Kidbwoy ambaye ndiye meneja wa msanii chipukizi, Barack De Prince, alisema muziki wa Tanzania unashindwa kufika anga la kimataifa kwa kuwa wasanii wengi si wabunifu na ni wavivu wa kufikiri.
“Wasanii wachanga ndio wanaonyesha kuzidi kubuni vitu vipya lakini wasanii wakongwe wanaotarajiwa kutangaza muziki wao kimataifa wamekosa ubunifu sasa watawezaje kufika huko mimi nasema hilo ni ndoto bila ubunifu hakuna mafanikio,” alisisitiza Kidbwoy.
“Zipo sababu lukuki za kwanini muziki wa Bongo unashindwa kufika mbali, lakini chache ni kutokana na wasanii wetu kutojifunza kutoka kwa wasanii wa nje waliofanikiwa, hivyo wasanii waache tabia ya kuiga bali wawe wabunifu kwa kuwa ndiyo siri ya mafanikio.”