28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

KICHWA CHA MTU ALIYE HAI KUPANDIKIZWA KWENYE MWILI MFU

Na JUSTIN DAMIAN


INAWEZA ikawa ngumu kuamini lakini itafanyika! Naam, operesheni ya aina yake itakayohusisha kukata kichwa cha mgonjwa na kukipandikiza kwenye mwili wa mtu aliyefariki kisha mgonjwa akawa mwenye afya tena.

Upasuaji huo utakaudumu kwa saa 36 na ambao utafanyika kwenye vyumba vya upasuaji vya kisasa zaidi duniani, utagharimu Pauni za Uingereza milioni 14 sawa na zaidi ya Sh bilioni 40 za Tanzania.

Atakayefanyiwa uhamishiwaji huo wa kiungo kipya ni Valery Spiridonov mwenye umri wa miaka 31, mgonjwa ambaye amekuwa akitumia kiti cha kutembelea  kutokana na matatizo ya misuli yanayomsumbua na kumfanya ashindwe kutembea.

Spiridonov anatarajia kupata tumaini jipya la maisha kutokana na operesheni hiyo atakayofanyiwa mwezi Desemba mwaka huu itakayohusisha kichwa chake kuwekwa kwenye mwili wa mtu aliyefariki na kumwezesha kutembea pamoja na kuendelea na maisha ya kila siku.

Mgonjwa huyu atakuwa ni wa kwanza kufanyiwa upasuaji huo ambao duniani inasuburi kwa hamu kuona matokeo yake.

Spiridonov raia wa Urusi ambaye ni mtaalamu wa kompyuta, amekubali kufanyiwa operesheni hiyo hatari zaidi kuwahi kufanyika.

Mtaalamu huyo wa kompyuta anasema ana matumaini makubwa na daktari wake ambaye amemwakikishia kuwa anaweza kukata kichwa chake akakiweka kwenye mwili wenye afya na kisha akaendelea na maisha

Si tarehe wala mahali ambapo upasuaji huo utafanyika pameshawekwa wazi lakini unatarajia kufanyika mwezi Desemba mwaka huu.

Akiongea katika mkutano wa waandishi wa habari, Spiridonov alisema taarifa zaidi zitakuwa zikitolewa kadiri muda utakavyokuwa unakwenda

Anasema; “bado naendelea kufanya mazungumzo na daktari wangu Sergio Canavero na baada ya muda mfupi atakuwa na habari nzuri kwa ajili ya umma.”

Mgonjwa huyo amekuwa akitawala vichwa vya habari vya vyombo vya habari mbalimbali duniani baada ya kukubali kufanyiwa opesheni hiyo ya aina yake

Spiridonov anasumbuliwa na ugonjwa wa Werdnig-Hoffman ambao umeathiri uti wake wa mgongo na kumfanya ashindwe kutembea, kupumua vizuri pamoja na kumeza chakula.

Wagonjwa wengi wanaopata maradhi ya aina hii, hupoteza maisha miaka michache baada ya kuzaliwa lakini yeye amekuwa ni mmoja kati ya asilimia 10 ambao huweza kufika umri wa utu uzima.

Hata hivyo, hali yake imekuwa ikibadilika kila kukicha na kuwa mbaya. Spiridonov aliwahi kuliambia gazeti la Mailonline kuwa, anataka kupata nafasi ya kuwa na mwili mpya kabla ugonjwa huo hujakatisha maisha yake.

Alisema, familia yake inaunga mkono wazo lake la kuwa binadamu wa kwanza kufanyiwa upasuaji huo. “Unapotaka kitu kifanyike, ni lazima ushiriki moja kwa moja,” anasema

Anaongeza, “nafahamu hatari iliyo mbele yake lakini nimeshafanya maamuzi. Hatuwezi kubashiri kwa usahihi nini kinaweza kutokea lakini nisingependa kuona anafanyiwa mtu mwingine wakati bado nipo hai,”

Mwili mpya utatoka kwa mtu aliyefariki na ambaye amekubali kujitolea mwili wake kabla ya mauti. Mtu huyo atakuwa amekufa ubongo lakini mwili wake una afya

Daktari atakayefanya upasuaji huo ameupa jina la ‘Heaven’ (mbinguni) ambao utahusisha kuunganisha sehemu mbili za miili tofauti na amesisitiza kuwa utaalamu pamoja na vifaa vya zoezi hilo vipo tayari

Kichwa cha mgonjwa kitawekwa kwenye mwili mpya kwa kutumia alichokiita Dk. Canavero ‘dawa ya maajabu’ ambayo ni kama gundi inayoitwa polyethylene glycol. 

Baada ya hapo, mgonjwa ataendelea kupatiwa matibabu kwa wiki nne wakati kidonda kikiendelea kupona huku akitakiwa kukaa bila kutembea.

Baada ya kipindi hicho, mgonjwa atatakiwa kuwa anajielewa ikiwa ni pamoja na kuongea kwa sauti yake ya mwanzo

Mgonjwa atapewa dawa maalumu zenye nguvu zitakilazimisha kichwa kuukubali mwili mpya. 

Watu wanaompinga Dk. Canavero wanasema amerahishisha namna ya kuunganisha uti wa mgongo na kusema kuwa zoezi hili ni kama ndoto za mchana

Hata hivyo, kama operesheni hiyo itafanikiwa, itatoa tumaini kwa mamia ya wagonjwa waliopooza na wenye ulemavu wa kudumu.

Spiridonov anatafuta fedha za kufanya uapasuaji kupitia jitihada zake binafsi kama kuuza zawadi pamoja na tisheti.

Amekuwa akiuza vitu kama saa za ukutani, kofia yenye nembo ya ‘Nia ya kuishi’ huku ikionyesha picha ya kichwa chake kikiwa kwenye mwili wenye afya.

Kwa mara ya kwanza opereshi ya aina hiyo ilifanyika kwa nyani miaka 45 iliyopita na nyingine ilifanyika kwa panya hivi karibuni nchini China.

Dk. Robert White alipandikiza kichwa cha nyani kwenye mwili wa nyani mwingine kwenye shule ya udaktari ya chuo kikuu cha Western Reserve nchini Marekani.

Hata hivyo nyani huyo alikufa baada ya siku nane kwa kuwa mwili ulikataa kichwa. Nyani huyo hakuweza kupumua mwenyewe wala kutembea kwa kuwa uti wa mgongo haukuweza kuungana vizuri na kichwa.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles