25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Kichuya: Maisha ya Misri ni bomba


ZAINAB IDDY

KWA miaka mitatu sasa Tanzania imekuwa ikipeleka nje ya mipaka yake wachezaji wengi wa soka, kwenda kucheza soka la kulipwa.

Kwa hili linalofanyika ni wazi soka la Tanzania linapiga hatua nyingine ya maendeleo.

Miongoni mwa wachezaji waliopata nafasi ya kusakata soka la kulipwa nje ya Tanzania ni kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya, aliyejiunga na klabu ya Pharco inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini Misri.

Pharco ilimnunua Kichuya kutoka Simba kwa dau la Sh milioni 196.

Mara baada ya kumalizana na Simba, Pharco iliamua kumtoa kwa mkopo Kichuya katika timu ya ENPPI inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo, lengo ni kupata uzoefu zaidi, kwani Pharco wapo mbioni kupanda daraja msimu ujao.

Kupata nafasi ya kukipiga Misri kunamfanya Kichuya aungane na Watanzania wengine; Himid Mao, anayeichezea Petrojet aliyojiunga nayo akitokea Azam FC na Yahya Zayd aliyejiunga na Ismaily akitokea Azam pia.

MTANZANIA limefanya mahojiano na Kichuya kutoka Misri ambaye anazungumzia maisha yake mapya ya kisoka nchini humo pamoja na matarajio yake kwa siku zijazo.

Hatua ya kucheza nje

Anasema alifurahi kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa.

Anasema siku aliyovaa jezi za ENPPI na kuingia uwanjani hakuamini, lakini anaumia kuona mambo si mazuri kwa kikosi chake hicho ndani ya dimba kwani hajawahi kupata ushindi tangu alipojiunga nacho.

 “Tangu nijiunge na kikosi hiki hatujapata ushindi, nilianza dhidi ya Al Ahly walipotufunga mabao 2-1, tukapoteza tena idadi kama hiyo kwa Zamaleck na kukubali kichapo kingine cha mabao 3-1 kutoka kwa Al Masry.

“Licha ya matokeo haya, bado nina matumaini tutapata tu ushindi japo roho inaniuma kuanza kwa vipigo, binafsi nitaendelea kujituma ili kuisaidia timu yangu.”

Anachokumbuka Tanzania

Kichuya anasema yapo mengi anayoyakumbuka ikiwemo familia yake, rafiki zake, watu wa Simba, lakini kubwa ni chakula akipendacho.

“Huku vyakula vipo vingi lakini aina ya upishi wao ni tofauti sana na huko nyumbani, yaani naweza kukwambia hapa nilipo nimeumisi sana  ugali na mlenda.

“Si unajua mimi ni Mluguru na chakula chetu cha asili ni ugali na mlenda wa bamia, huku sijakutana nacho kabisa nimepanga nikirudi tu nitakula hadi hamu imalizike,” anasema.

Masilahi

“Huku mchezaji ana thamani tofauti na Tanzania, nashukuru Mungu tangu nije nimeweza kulipwa mshahara wangu kwa wakati na kutuma wote nyumbani kwa kuwa napata mahitaji yote muhimu.

“Sasa hivi mshahara wangu umepanda tofauti na nilivyokuwa nyumbani kwani kwa mwezi nina uhakika wa kupata zaidi ya milioni 15 ambao ni zaidi ya mara tatu ya kile nilichokuwa naupata Simba na kama nitaendelea kujituma bila shaka thamani yangu itapanda,” anasema Kichuya.

Lugha

Kiukweli lugha ninayoifahamu kiufasaha ni Kiswahili, Kiingereza naibia ibia maneno machache baada ya kufanya kazi na makocha wageni.

“Nakubali lugha kwangu ni tatizo, lakini nashukuru, huku tofauti na nyumbani wapo watu maalumu ambao wanatutafsiria kile anachozungumza kocha, si mimi peke yangu ninayesumbuliwa na hili kuna wengine pia hawajui Kifaransa au Kigereza kinachotumiwa na kocha wetu.”

Siri ya mafanikio

“Ukiachilia mbali ushauri niliokuwa naupata kwa walionitangulia katika soka mfano Mbwana Samatta ambaye alipokuja likizo na kuona kiwango changu kipo chini tulipokuwa tunacheza na Kagera Sugar, baada ya mchezo aliomba kuzungumza na mimi ili ajue nina tatizo gani.

“Baada ya kumweleza kuwa sina matumaini ya kucheza soka la kulipwa, alinisihi nisikate tamaa kwani kufanya hivyo ni kuukaribisha umasikini, toka hapo nikapata nguvu mpya hatimaye leo hii nipo huku.

“Lakini pia juhudi zangu ndizo zilizonifikisha hapa leo, Simba nilikuwa napata nafasi ya kucheza mechi za kitaifa na kimataifa jambo lililozivutia timu zaidi ya tatu zilizoleta ofa Simba, lakini niliona hapa ndiyo sehemu sahihi kwa sasa,” anasema.

Matarajio

“Nina miaka mitatu tu ya kufanya kazi Misri, baada ya hapo nataka niende kucheza sehemu nyingine, nitafurahi kama nitakuwa napanda dau kila mwaka.

“Najituma ili baada ya muda niliojiwekea niwe nimepanda thamani ikiwezekana mara tatu ya nilivyonayo sasa, mpira ni kipaji changu hivyo sitaki kuona nashindwa kutimiza malengo niliyoyaweka tangu natoka nyumbani kwetu,” anamaliza Kichuya ambaye wakati anaichezea Simba alisifika kwa kuwa na bahati ya kuifunga Yanga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles