26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Kichere awa CAG mpya

Andrew Msechu -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amemteua Charles Kichere kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Profesa Mussa Assad.

Kichere ambaye aliwahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kabla ya kupangiwa majukumu mengine Juni 8, mwaka huu na nafasi yake kuchukuliwa na   Edwin Mhede.

Novemba 20,2016, Rais Dk. Magufuli alimteua Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA na Machi 25,2017 akateuliwa kuwa Kamishna Mkuu akichukua nafasi ya Alphayo Kidata.

Kichere alikuwa mtu wa nne kung’olewa kwenye kiti hicho ndani ya miaka minne, akitanguliwa na Rished Bade, Kidata na Dk. Philip Mpango.

Kutokana na kutenguliwa kwa uteuzi wake, Rais Dk. Magufuli alimteua kwa nafasi nyingine na kumpeleka kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Kichere ametumikia nafasi hiyo kwa takribani miezi mitano, hadi uteuzi wa jana ulipofanyika.

Akitangaza uteuzi huo jana, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi,  alisema Rais Dk. Magufuli, amefanya uteuzi wa kujaza nafasi ya Profesa Assad ambaye muda wake wa miaka mitano unamalizika leo, Novemba 4.

“Kichere anachukua nafasi hii kuanzia tarehe 4 mwezi wa 11, akichukua nafasi ya Profesa Assad ambaye muda wake wa miaka mitano unakwisha kesho (leo) tarehe 4 mwezi wa 11, 2019. Kabla ya uteuzi huo Kichere alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe,” alisema Balozi Kijazi.

KAULI YA KICHEERE

Alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia uteuzi huo, Kicheere alisema “Namshukuru Mungu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na imani na kuniteua kwenye nafasi hii”

Kuhusu nini anawambia Watanzania alisema “Nitasema kesho (leo), baaa ya kuapishwa, niko njiani hatuwezi kuelewana kwa simu”

Waliowahi kuwa ma-CAG

Kichere anakuwa CAG wa saba nchini tangu Uhuru, baada ya R.W.A. McColl mwaka 1961 hadi 1963, Gordon Hutchinson mwaka 1964 hadi 1969, Mohamed Aboud mwaka 1969 hadi 1996, Thomas Kiama mwaka 1996 hadi 2005, Ludovick Utouh mwaka 2006 hadi 2014 na Profesa  Mussa Juma Assad mwaka 2014 hadi 2019

Wasifu wa Kichere

Kichere ana Shahada ya Sheria (LL.B) kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es salaam Tanzania, Shahada ya Uzamili ya Utawala wa Biashara (MBA) katika Fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Diploma katika Usimamizi wa Fedha wa Miradi iliyofadhiliwa na wafadhili kutoka Kituo cha African Renaissance, Mbabane Swaziland, Shahada ya Biashara katika Uhasibu (B.Com Uhasibu) Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Yeye ni mwanachama wa Kamati za Mikopo na Ukaguzi.

Amekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe (RAS) hadi uteuzi mpya uliofanyika na Kamishna Mkuu wa zamani katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Pia amewahi kuwa Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkuu wa Fedha na Mhasibu Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS), Mhakiki Mkuu wa Ndani wa Wakala wa Barabara za Tanzania (TANROADS), Mkaguzi wa Ndani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkaguzi wa Ndani wa Kampuni ya Chai ya Unilever Tanzania Limited na Mkaguzi wa ndani / Mweka Hazina wa Kampuni ya Unilever Limited Kenya.

Mvutano Prof. Assad na Bunge

Kabla ya Rais Dk. Magufuli, kutengua uteuzi wa Assad jana, Aprili 2, mwaka huu, Bunge la Tanzania lilitangaza azimio la kutofanya kazi na CAG, Profesa Assad baada ya kumtia hatiani kwa kauli yake ya kusema chombo hicho ni dhaifu wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Umoja wa Mataifa (UN). 

Profesa Assad alitoa kauli hiyo katika mahojiano na Idhaa hiyo nchini Marekani na kusema Bunge la Tanzania halina meno na ni dhaifu kwa sababu limeshindwa kushughulikia mapendekezo ya ripoti za ubadhirifu zinazotolewa na ofisi yake.

Kutokana na kauli hiyo, Aprili 2, Bunge lilifikia hatua ya kukataa kufanya naye kazi, baada ya Kamati ya Maadili ya Bunge Haki na Madaraka ya Bunge kuliomba Bunge kuridhia kutofanya kazi na CAG kwa sababu ameshusha hadhi ya Bunge kwa kauli zake. 

Akisoma ripoti ya Kamati iliyomhoji CAG Assad Januari 21 mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Emanuel Mwakasaka alisema wakati Profesa Assad anahojiwa na kamati hiyo alionyesha dharau na hakujutia kauli yake. 

Alisema bila kupima athari yake wakati akizungumza katika redio ya kimataifa alikosa uwajibikaji wa pamoja na hiyo ni tabia mbaya kwasababu alikataa kuomba msamaha mbele ya wajumbe wa kamati.

“Kamati ya Maadili ya Bunge tulimuuliza CAG Assad kama ataacha kulitumia neno udhaifu akasisitiza ataendelea kulitumia na hakujutia kulitumia dhidi ya Bunge,” alisema Mwakasaka. 

Alisema CAG ni mteule wa Rais na kutokana na kadhia hiyo, Bunge haliko tayari kufanya kazi naye na haliko tayari kushirikiana naye kutokana na majukumu yake. 

Pia Kamati hiyo ilipendekeza Bunge kumsimamisha mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kuhudhuria mikutano miwili ya Bunge kuanzia tarehe ya azimio hilo kutokana na kuunga mkono kauli ya CAG, Profesa Mussa Assad kuwa Bunge ni dhaifu ambapo Mdee alihojiwa na kamati hiyo kwa kauli hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson aliagiza Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa kutamka bungeni kuwa Bunge ni dhaifu.

ACT Wazalendo walaani

Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari muda mfupi baada ya uteuzi wa Kicheere jana, Chama cha ACT Wazalendo kilisema kwa mara nyengine Katiba ya nchi imevunjwa ilhali aliyepo bado anapaswa kuendelea kuwa madarakani.

Katika taarifa hiyo, iliyotolewa na Mratibu Mawasiliano ACT Wazalendo Taifa, Mbarala Maharagande, ilisema Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye pia amewahi  kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali ( PAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (POAC)  kwa mwaka 2007-2015, ameleza kusikitishwa kwake na hatua ya kuondolewa kwa Profesa Assad.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya Ukaguzi ya Taifa ya mwaka 2008 muda wa kukaa madarakani wa CAG ni vipindi viwili vya miaka mitano mitano, isipokuwa tu kama CAG ametimiza umri wa  miaka 65 na kama hakuna masuala ya nidhamu kwa mujibu wa Katiba, CAG ni lazima ahudumu kwa mihula miwili, lakini huyo amehudumu muhula mmoja tu na kwa sasa ana miaka 58.

Teuzi nyingine

Alisema katika uteuzi wake, Rais Dk. Magufuli pia amemteua Katibu Tawala wa Mkoa ambapo amemteua Katarina Revocati kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Kabla ya uteuzi huo, Katarina alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania na kwa sasa anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kichere ambaye amepata uteuzi mpya.

Uteuzi wa tatu,ni wa Balozi, ambapo Rais amemteua Mhandisi Aisha Amour aliyekuwa Katibu Tawala wa Kilimanjaro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, baada ya kupewa hadhi ya ubalozi Septemba, mwaka huu.

Dk.Kijazi alisema uteuzi wa nne ni wa Kamishna wa Kazi ambapo Rais Magufuli amemteua Kanali Francis Mbindi kuwa kamishna wa kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Gabriel Malata ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.

Alisema Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa majaji 12 wameteuliwa kuwa majaji wa mahakama Kuu.

Alisema majaji hao, ni Dk Zainab Mango ambapo kabla ya uteuzi alikuwa Wakili wa Serikali Mkuu katika Ofisi ya Taifa Mashtaka.

Mwingine ni Edwin Kakolaki ambaye kaba ya uteuzi huo aklikuwa katika Ofisi ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini.

Alisema mwingine Dk. Deo Nangela, ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa ofisi ya Tume ya Ushindani.

Alisema mwingine, ni Frederick Manyanda ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashtaka.

Mbali na hao pia Elizabeth Mkwizu ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Alisema mwingine, ni Augustine Rwizile ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama.

Mwingine ni Ephery Sedekia ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwingine ni Angaza Mwaipopo ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisi ya Rais, Ikulu.

Dk. Kijazi, alisema mwingine ni Joakim Tiganga ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Kassim Robert ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa mitengo cha kudhibiti fedha haramu katika Wizara ya Fedha.

Alisema mwingine ni Said Kalunde ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwingine ni Angela Bahati ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Msaidizi Tume ya Kurekebisha Sheria.

Alisema wateule hao pamoja na  Mwenyekiti, makamu mwenyekiti na makamishna watano wa Tumemya Haki za Binadamu na utawala Bora ambao Rais aaliwateua hivi karibuni wataapishwa leo Jumatatu Novemba 4, saa 3.30 asubuhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles