Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM
NI dhahiri sasa kibano cha kodi ya ardhi kinahamia kwa mashirika ya umma na taasisi nyingine baada ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kutangaza kuwa Juni 11 atakutana na mashirika ya umma 207 yanayodaiwa kodi ya pango la ardhi.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na wizara hiyo jana, ilisema Lukuvi atakutana na mashirika hayo katika kikao maalumu alichokiitisha ikiwa ni mkakati wa wizara hiyo kuhakikisha wadaiwa wote wa kodi ya ardhi wanalipa kwa mujibu wa sheria.
“Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dorothy Mwanyika, Lukuvi atakutana na mashirika na taasisi hizo jijini Dodoma.
Taarifa hiyo ilisema pia taasisi, wenye viwanda na maeneo makubwa ya biashara ambao wana malimbikizo makubwa ya kodi ya pango la ardhi, watatakiwa kufika katika kikao hicho maalumu bila kukosa wakiwa na nyaraka za umiliki pamoja na stakabadhi za malipo ya kodi ya pango la ardhi waliyofanya.
Ilisema wadaiwa watakaoshindwa kufika katika kikao hicho, hatua za kufuta miliki zao na kuuza maeneo husika zitafuata kwa mujibu wa sheria ya ardhi, sura namba 113, kifungu cha 50.
Ilitaja baadhi ya taasisi na mashirika yaliyopewa wito wa kuhudhiria kikao hicho kuwa ni Shirika la Ndege Tanzania (ATC), Arusha International Conference Center (AICC), Bodi ya Pareto, Chuo cha Madini, Bodi ya Korosho, BP Tanzania Ltd-Puma Energy, Chuo cha Ushirika, CRDB, Mamlaka ya Maji Dodoma (Duwasa), Kahama Mining Corporation na Kituo cha Elimu Kibaha.
Mengine ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHF), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Rubada-Wizara ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Mzumbe, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Capco Tanzania Ltd, Aga Khan Foundation, Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Exim Bank Tanzania na Shirika la Masoko Kariakoo.
Taarifa hiyo ilisema uamuzi wa Lukuvi kukutana na wadaiwa sugu hao wa kodi ya ardhi, ni mwanzo wa jitihada za wizara hiyo kuhakikisha wanalipa kabla ya Juni 30.
Ilisema baada ya tarehe hiyo kupita, watakaokaidi watafikishwa katika mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya ambako adhabu yake ni kufuta miliki na kuuza maeneo husika kufidia deni.