31 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 3, 2023

Contact us: [email protected]

Kibano kipya madereva bodaboda chaja

Na TUNU NASSOR

-DAR ES SALAAM

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inakusudia kupeleka muswada bungeni utakaowabana madereva wa pikipiki za kubeba abiria, maarufu bodaboda kuwa na bima ya afya kabla ya kupewa leseni ya kutoa huduma kutokana na ongezeko la ajali.

Akizugumza Dar es Salaam jana wakati wa ufunguzi wa kambi ya utoaji wa miguu bandia kwa watu 600 katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema sababu ya kusudio hilo ni wingi wa ajali zitokanazo na bodaboda na kuongeza mzigo wa gharama za matibabu kwa sekta ya afya.

Ummy alisema taasisi hiyo kwa mwezi imekuwa ikipokea majeruhi 700 hadi 900 wa ajali za barabarani, idadi ambayo imekuwa ikiongezeka kila siku.

Alisema awali kabla ya kuruhusu pikipiki kuwa chombo cha usafirishaji wa abiria, MOI ilikuwa ikipokea majeruhi wa ajali 400 hadi 600 kwa mwezi.

“Nimeongea na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumwomba watafute jinsi ya kudhibiti pikipiki hizo, kwani zimekuwa zikibeba zaidi ya abiria wawili hadi watatu, nimemuomba kabla dereva bodaboda hajapewa leseni, sharti la kwanza awe na bima ya afya ndio apatiwe leseni ya udereva,” alisema Ummy.

Alisema bima ya afya ni muhimu kwa sababu gharama za matibabu mtu anapopata ajali ni kubwa na zinaongeza mzigo katika sekta hiyo.

“Gharama za upasuaji mdogo katika Taasisi ya MOI ni Sh 200,000 na kupatiwa mguu bandia inagharimu Sh milioni 1.5 hadi 3 jambo ambalo ni mzigo mkubwa kwa sekta ya afya,” alisema Ummy.

Aidha alisema kambi ya upimaji wa watu wanaotakiwa kupatiwa miguu bandia, waliojiandikisha walikuwa 900 na waliofanikiwa kupewa miguu hiyo ni 600, hivyo ameahidi kutafuta njia nyingine ya kuwapatia miguu hiyo watu 300 waliobaki.

“Tumefanikiwa hili kwa kushirikiana na Ubalozi wa India ambao umekuwa mstari wa mbele kuchangia sekta ya afya, ambapo mwaka jana walichangia dawa zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni mbili na wameahidi tena kutoa fedha hizo mwaka huu, ambapo dawa za Sh milioni 500 watapewa MOI,” alisema.

Alisema ameona dawa za Sh milioni 500 wapewe MOI kwa sababu amekuwa akiridhika na huduma zinazotolewa katika taasisi hiyo licha ya kuwa na baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo.

Aidha Ummy aliwahakikishia MOI kuwa Serikali itaendelea kutatua changamoto zilizopo kwa wakati ili waendelee kutoa huduma zinazokidhi mahitaji ya wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi wa MOI, Charles Mkonyi aliishukuru Serikali kwa kuwezesha upatikanaji wa huduma pamoja na kufunga vifaa vya kisasa vya uchunguzi.

“Tunaomba kusaidiwa upanuzi wa eneo la mazoezi kwa sababu kwa sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wenye mahitaji hayo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles