30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

KIBANO KIPYA CHAJA VYETI FEKI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imesema watumishi wa umma waliobainika kuwa na vyeti feki lakini wamenufaika wa mikopo ya elimu ya juu, wanapaswa kulipa madeni yao.

Imesema hadi sasa imekusanya Sh bilioni 216.9 kati ya Sh bilioni 427.7 zilizoiva na kwamba asilimia 65 ya mikopo iliyokusanywa inatoka kwenye sekta ya umma na asilimia 35 sekta binafsi.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdulrazaq Badru, alisema watatumia njia mbalimbali kuhakikisha wadaiwa hao wanapatikana na kulipa madeni yao.

Mkurugenzi huyo alisema kama wadaiwa hao wasipopatikana, wadhamini wao watawajibika kuwatafuta na kuhakikisha wanalipa madeni wanayodaiwa na ikibidi watawajibika kisheria.

“Kama kuna wanufaika walibainika kughushi vyeti vya elimu, lakini pia walinufaika na mkopo wetu, bado wana wajibu wa kisheria kurejesha mikopo wanayodaiwa. Hata mwanafunzi aliyeshindwa kuendelea na masomo chuoni (disqualified) analazimika kulipa mkopo aliokopeshwa.

“Tumedhamiria kuhakikisha kila aliyekopa kama hajafariki dunia lazima arejeshe fedha anazodaiwa na asipopatikana mdhamini atawajibika,” alisema Badru.

Alisema pia wameingia makubaliano na taasisi zinazotunza taarifa za wakopaji (CRB) ili kuwabaini wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu na kuhakikisha hawakopesheki sehemu nyingine hadi walipe madeni yao.

Kuhusu wadaiwa sugu, alisema hadi kufikia mwaka jana, walikuwa 142,470 wenye mikopo ya Sh bilioni 239.3 iliyoiva na kati yao 45,000 wamejitokeza na wengine wanaendelea kutafutwa.

Alisema pia katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 waajiri 2,136 walikaguliwa na kupitia hatua hiyo, wanufaika 45,960 walibainika na kurejesha mikopo ya Sh bilioni 54.7.

Hata hivyo, alisema baadhi ya waajiri wamekuwa hawatoi ushirikiano wa kutosha, kwamba wamekuwa wakitoa taarifa ‘feki’ kuhusu waajiriwa wao, kutokata makato na kushindwa kuwasilisha kwa wakati mwafaka na kutotoa taarifa za waajiriwa waliohama au kuacha kazi.

Alisema mwaka jana walizishtaki kampuni tatu kwa kushindwa kuwasilisha makato ya waajiriwa wao ambao wanadaiwa na bodi.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo, Phidelis Joseph, alisema kila mwajiri anatakiwa kutuma taarifa za mwajiriwa mpya ndani ya siku 28 ili bodi ihakiki kujua kama anadaiwa.

Utaratibu huo mpya wa kuwasaka waliopatikana na vyeti feki ili walipe madeni yao ni pigo jingine ambalo linakwenda mbali zaidi kutokana na baadhi ya wadhamini wa wanafunzi huwa ni wazazi wao.

Mwisho.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles