24.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 8, 2022

KIBA, DIAMOND MTV MAMA LEO…. Nani atasepa na kijiji?

nini

Na CHRISTOPHER MSEKENA

MACHO na masikio ya mashabiki wa Bongo Fleva, leo yameelekezwa bondeni kwa mzee Madiba katika Jiji la  Johannesburg, Afrika ya Kusini ambapo Tuzo za MTV Africa Music Awards (MTV MAMAs 2016) zinatolewa, huku wababe wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz na Ali Kiba wakikutana.

Kiba na Diamond ni miongoni mwa wasanii wanaowania tuzo hizo ingawa wapo katika vipegele tofauti, lakini habari ya kufurahisha zaidi ni kwamba, wote watapanda jukwaa moja kwa ajili ya kutumbuiza.

Je, nani ataonyesha umwamba? Hilo ndiyo swali linalozunguka kwenye vichwa vya mashabiki wa wasanii hao kwa sasa.

Diamond anawania tuzo mbili, Msanii Bora wa Kiume na Msanii Bora wa Mwaka, huku Kiba akisimama kwenye kipengele cha Tuzo ya Kolabo Bora kupitia wimbo wa Unconditionally Bae aliofanya na Sauti Sol.

Waandaaji wa tuzo hizo zilizoanza kutolewa mwaka 2008, bila shaka wamezingatia uwezo na ushindani mkubwa walionao wasanii hao kiasi cha kuamua kuwakutanisha katika jukwaa moja.

Ni kawaida ya Kiba na Diamond kuvunja historia pale wanapokutanishwa jukwaa moja. Ni adimu sana  kushuhudiwa onyesho lao na pale unaposhuhudia live au runingani, lazima utakiri kuwa hawa ndiyo wasanii ghali na wenye mvuto mkubwa kwa sasa.

UNAIKUMBUKA FIESTA 2014?

Baada ya kutambiana ubabe kwa muda mrefu kuhusu nani ndiye mmiliki rasmi wa kiti cha ufalme, wakali hawa walikutana kwenye jukwaa moja la shoo ya Fiesta katika Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Kiba alikuwa akitamba na kitu cha Mwana, wakati Diamond akinesanesa jukwaani na Remix ya ngoma yake Number One akiwa amemshirikisha Davido, staa wa Nigeria.

SURPRISE YA KING KIBA MOMBASA

Ulipita muda wawili hawa hawajakutana jukwaa moja lakini Septemba 10, mwaka huu walijikuta wapo jukwaa moja katika sherehe za chama cha ODM, jijini Mombasa nchini Kenya.

Awali, matangazo yalitangaza kuwa Diamond ndiye msanii pekee wa Bongo Fleva atakayetumbuiza katika sherehe hizo lakini ghafla hali ya Viwanja vya Mama Ngina Drive vilichafuka kwa shangwe pale MC alipomtangaza King Kiba kuwa atapanda jukwaani.

NANI KUSEPA NA KIJIJI LEO?

Timu za Kiba na Diamond bado zipo kwenye mvutano mkali kutokana na madai ya Kiba kuhisi kufanyiwa figisu na meneja wa Diamond, Sallam Sk kwenye Tamasha la Mombasa Rocks Music, lililofanyika hivi karibuni mjini Mombasa.

Kiba anahisi hujuma baada ya kuzimiwa mic wakati akiwa jukwaani anapafomu ambapo Sallam Sk alikuwa nyuma ya jukwaa.

Wakati joto la sakata hiyo halijatulia, uongozi wa MTV Base umewapanga kutumbuiza jukwaa moja, jambo ambalo kwa hakika litamaliza ubishi wa nani mbabe.

Hii itakuwa mara ya tatu kwao kukutana jukwaa moja. Kiba yeye ni mara yake ya kwanza kutumbuiza na kushiriki tuzo hizo, lakini Diamond ameshapanda katika jukwaa hilo  mwaka juzi akiwa na Davido.

Kadhalika mwaka jana aliondoka na Tuzo ya Mtumbuizaji Bora. Uadimu wao kukutana jukwaa moja unaibua msisimko wa aina yake na hivyo wengi kusubiri na kuona nani mbabe.

BONGO FLEVA IMO SANA TU

Mbali na Kiba na Diamond, wapo wasanii wengine wa Bongo Fleva ambao wanawania tuzo hizo. Msanii mkali wa kike,   Vanessa Mdee yeye anawania Tuzo ya Msanii Bora wa Kike, wakati Navy Kenzo wakiwa kwenye Tuzo ya Kundi Bora.

Msanii mwingine anayetuwakilisha Watanzania katika tuzo hizo ni Rayvan ambaye yupo katika kipengele cha Msanii Bora Chipukizi.

Tunawatakia kila la kheri wasanii wetu, warudi nyumbani na tuzo zote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,235FollowersFollow
549,000SubscribersSubscribe

Latest Articles