30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Khamis Mgeja awaangukia viongozi waastafu

Khamis Mgeja
Khamis Mgeja

NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

VIONGOZI wastaafu nchini wametakiwa kujitokeza  kuwashauri viongozi waliopo madarakani, kuhakikisha wanailinda na kuisimamia Katiba ya nchi ili isivunjwe.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Taasisi ya Wazalendo, Khamis Mgeja, alisema hivi sasa Taifa linapita kwenye wakati mgumu tofauti na miaka 30 iliyopita, hivyo ni muda mwafaka kwa marais wastaafu na viongozi mbalimbali kujitokeza kukemea viashiria vya uvunjwaji wa Katiba.

Alisema kuna mambo yanaonesha Rais Dk. John Magufuli anakiuka Katiba, hivyo ni wakati mwafaka kwa viongozi wastaafu kukemea jambo hilo, vinginevyo Taifa litaelekea kubaya.

“Tulitegemea Rais Dk. Magufuli,  ataisimamia Katiba ipasavyo na kuilinda kama alivyoapa lakini kuna mambo anayafanya yanakiuka Katiba huku akitambua hakuna aliye juu ya sheria. Jambo hili linahitaji viongozi wastaafu kukemea kabla halijaota mizizi,” alisema Mgeja.

Alisema migogoro baina ya baadhi ya vyama vya siasa na Serikali ni viashiria vibaya kwani wananchi wakishindwa kudai haki kwa  mazungumzo, wataandamana.

“ Tunaomba marais wastaafu akina Benjamin Mkapa, Ally Hassan Mwinyi, Dk. Jakaya Kikwete na viongozi mbalimbali wastaafu na wa kidini wahakikishe wanajitokeza kuisimamia Katiba ili isivunjwe vingine historia itawahukumu kwa kushindwa kusimamia Katiba  ikiwemo suala la kuwaonya viongozi wanaoikiuka ,”alisema Mgeja.

Alisema ni vyema viongozi wastaafu wakaacha kusubiri mambo yaharibike ndipo wajitokeze kinachotakiwa ni kushauri haki itendeke na wasimfurahishe mtu kwa ukimya wao.

“ Nakumbuka Juni 14, mwaka 1995 Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kutamka kuna nyufa inahitajika kuzibwa ya kuchezea Katiba na sheria ya vyama vya siasa  kwa gharama yoyote ushirikiano unahitajika huku akisisitiza rais aliyeapa kuilinda Katiba hiyo anapaswa kuilinda na si kuionea aibu,” alisema Mgeja.

Alisema kiongozi yeyote atakayeona aibu kukemea vitendo vya uvunjwaji sheria hafai kuwepo madarakani hivyo ni muda muafaka kwa viongozi wastaafu kuiga mfano wa Nyerere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles