23 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Kesi zaanza kuiandama Boeing

NEW YORK, MAREKANI

FAMILIA ya Jackson Musoni, ambaye ni mmoja wa abiria waliofariki dunia kwenye ajali ya Shirika la Ndege la Ethiopia, imefungua mashtaka dhidi ya Kampuni ya utengenezaji ndege ya Boeing nchini Marekani.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya watu wote 157 waliokuwa ndani ya ndege hiyo kufariki katika ajali iliyotokea mapema mwezi huu.

Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, ndugu wa Jackson, ambaye alikuwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa na raia pekee wa Rwanda aliyekuwamo kwenye ajali hiyo, wanadai kuwa ndege sampuli ya Boeing 737 Max zina mapungufu ya kiusanifu katika mifumo yake ya kujiendesha.

Ndege zote 371 zinazomilikiwa na mashirika mbalimbali za aina ya 737 Max zimepigwa marufuku kuruka toka ilipotokea ajali hiyo, ambayo ilikuwa ni ya pili kwa sampuli hiyo ndani ya miezi mitano.

Ajali ya kwanza ilitokea Oktoba mwaka 2018 nchini Ethiopia na kuua watu wote 181 waliokuwamo ndani ya ndege hiyo. Hadi sasa kampuni ya Boeing bado haijatoa tamko lolote kuhusiana na kesi hiyo.

Wachunguzi pia bado hawajatoa ripoti kamili juu ya sababu hasa ya ajali hiyo. Kampuni ya Boeing katikati ya wiki hii ilitangaza kuwa wamefanyia marekebisho mfumo wa udhibiti (MCA) ambao unahusishwa na ajali zote mbili za ndege zake.

Kama sehemu ya kuboresha ndege hizo, Boeing itaweka mfumo wa hali ya hatari kulingana na viwango, ambao awali ulikuwa si wa lazima.

Ndege zilizopata ajali za makampuni ya Lion Air ya Indonesia na Ethiopian Airlines, hazikuwa na mfumo wowote wa kuashiria hali ya hatari, ambao lengo lake ni kuwaonya marubani wakati mtambo wa uongozaji wa safari ya ndege unapotoa taarifa kinyume cha matarajio.

Boeing imesema makampuni hayatakuwa yakitozwa fedha za ziada kwa ajili ya kuweka mfumo huo wa usalama wa ndege hizo. Lakini haijajulikana ni lini ndege hizo zilizozuiwa kusafiri kote duniani mwezi huu zitaruhusiwa kupaa.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Boeing kukubali kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiufundi kwenye ndege hizo. Awali mamlaka za Marekani zilitetea kampuni hiyo, zikidai sampuli 737 Max ni salama.

Shinikizo kubwa la kimataifa dhidi ya ndege hizo lilianza mara tu baada ya ajali ya Ethiopia kutokea. Nchi kadhaa, ikiwamo za Jumuiya ya Ulaya, Canada, China na Rwanda zilipiga marufuku ndege hizo kupaa kwenye anga za mataifa hayo.

Katika ajali hizo, raia waliofariki kwenye ajali ya Ndege Ethiopia ni kama ifuatavyo; Kenya (32),  Canada (18), Ethiopia (9), Italia (8), China (8), Marekani (8), Uingereza (7), Ufaransa (7), Misri (6), Ujerumani (5),   India (4), Slovakia (4), Australia (3), Uswizi (3), Urusi (3),  Comoro (2), Hispania (2), Poland (2), Israeli (2), Ubelgiji (1), Indonesia (1), Somalia (1), Norway (1),   Serbia (1), Togo (1), Msumbiji (1), Rwanda (1), Sudan (1), Uganda (1), Yemen (1).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,800FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles