26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

KESI ZA UJAUZITO ZIPELEKWE MAHAKAMANI -DC

Na IBRAHIM YASSIN -NKASI


MKUU wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Said Mtanda, ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi wilayani humo kuhakikisha kesi zote zinazohusu wanafunzi kupata ujauzito zaidi ya 50 zilizopo zifikishwe mahakamani.

Agizo hilo amelitoa juzi, wakati wa kikao cha Maraza la Madiwani.

Alisema ameshtushwa na taarifa zilizotolewa katika baraza hilo na kubainika kuna kesi za siku nyingi za mimba shuleni ambazo zimekwama polisi na hazijawahi kufikishwa mahakamani.

Alisema kazi ya polisi ni kukamata au kupokea mashtaka na kuyapeleka mahakamani na akahoji ni kwa nini kesi hizo zimekwama polisi na kudai kuwa atataka maelezo ya kina juu ya hilo.

“Haiwezekani mtu kampa mimba mwanafunzi, kesi inakaa inakwama polisi muda mrefu bila kwenda mahakamani, huko ni kwenda kinyume cha agizo la waziri mkuu juu ya wale wote wanaowapa mimba wanafunzi,” alisema Mtanda.

Alisema suala la mimba si jambo la mchezo, lakini anashangazwa na Jeshi la Polisi wanavyozishughulikia kesi hizo.

Alisema inawezekana kuna kitu ndani yake, haiwezekani kesi zote ziishie polisi wakati mahakama ndicho chombo pekee chenye uwezo wa kumtambua mkosaji.

Katika hatua nyingine, amezitaka mamlaka katika ngazi ya vijiji na kata kuhakikisha wamechukua hatua dhidi ya utoro kwa watoto wa shule za msingi na sekondari, ambapo kuna watoto zaidi ya 200 ambao hawaendi shule bila sababu za msingi.

Alisema serikali za vijiji zina jukumu kubwa la kuhakikisha mahudhurio ya watoto yanakuwa mazuri.

Lakini pia, aliwaonya viongozi wa vijiji kuacha mara moja kuzigeuza ofisi zao kuwa mahakama, bali wajitahidi kufuata utaratibu kwa kesi zote zinazohitaji utaratibu wa kisheria.

Alidai kuna taarifa kuwa, hivi sasa kuna baadhi ya maofisa watendaji wa vijiji wamekuwa wakitoa hukumu katika ofisi zao na kuwatoza watu faini hadi ya Sh 1,000,000 kinyume cha sheria.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Wilbroad Chakukile, aliwataka madiwani kuzisimamia serikali za vijiji ili ziweze kufuata sheria na kanuni kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo na si vinginevyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles