DERICK MILTON-SIMIYU
ASASI isiyokuwa ya Kiserikali inayotoa Msaada wa Kisheria (LSF), imeshangazwa kukutana na kesi za ardhi zilizochukua muda mrefu mahakamini katika Mkoa wa Simiyu, huku moja ya kesi hizo ikiwa na miaka 55 na bado haijatolewa hukumu.
Mbali na kesi hiyo, asasi hiyo pia imeeleza kuwa imekutana na kesi nyingi ambazo zilianza muda mrefu, walalamikaji wakiwa bado wadogo lakini sasa wamekuwa wazee na bado hazijatolewa hukumu.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa asasi hiyo, Scholastica Jullu, wakati wa kilele cha wiki ya msaada wa kisheria kitaifa iliyokuwa ikifanyika mjini Bariadi mkoani Simiyu.
Alisema sababu kubwa ambayo wamegundua kwa kesi hizo kuchukua muda mrefu bila ya kutolewa hukumu, ni walalamikaji kutokufuata utaratibu wa kufungua mashauri sehemu sahihi.
“Kuna kesi moja ina miaka 55 mahakamani, ni kesi ya ardhi mpaka leo haijafika mwisho, lakini tumekutana pia na watu kesi yao ilianza tangu wakiwa watoto lakini leo ni wazee bado haijamalizika,”aliongeza Jullu.
Alisema walichogundua katika wiki hiyo, bado elimu ya kisheria inahitajika kwa kiwango kikubwa kwa wananchi pamoja na wasaidizi wa kisheria.
“Tumebaini kuwa wananchi wengi wamekuwa hawana uelewa wa sehemu ipi sahihi kesi zao za ardhi zinatakiwa kuanzia au ngazi gani waanzie ili waweze kupata haki yao kwa wakati,”alisema Jullu.
Mbali na hilo, Jullu alisema kuwa wamekutana na kesi nyingi ambazo zimetolewa maamuzi, lakini bado hukumu haijakazwa.
“Kuna kitu kinaitwa kukazia hukumu, walalamikaji wengi kesi zao za ardhi zimefika mwisho kwa maana ya kutolewa hukumu, lakini zile hatua za kukuza hukumu bado hazijafanyika na mlalamikaji kubaki anahangaika,”alieleza Jullu.
Kwa upande wake, Ofisa Programu kutoka Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Grolia Baltazar alisema kuwa kesi nyingi ambazo zinahusu migogoro ya ardhi zinatokea pale baba wa familia anapofariki.
Alisema katika familia ambazo mama ametangulia mbele za haki, migogoro hiyo haijitokezi, hali ambayo alisema elimu ya kuandika wosia inahitajika zaidi kwa wananchi.
Naye, Msajili wa Watoa Huduma wa Msaada wa Kisheria, Felister Mushi kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, alisema kwa muda wa wiki moja wametoa huduma kwa watu zaidi ya 1000.
“Kwa watu wote hao wengi walikuwa na kesi za ardhi, lakini nyingi zipo mahakamani, tumegundua elimu ya kisheria inahitajika zaidi kwa wananchi,”alisema Mushi.
Akifunga maazimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka alizitaka asasi za msaada wa kisheria kwenda zaidi kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini kwa ajili ya kuwapatia elimu ya sheria mbalimbali.
“Kuna idadi kubwa ya wananchi vijijini hawajui wafanye nini pale wanapopata tatizo, ni vyema asasi zikajikita zaidi kwa wananchi wa vijijini ambao hawana uelewa wowote na ndiyo wenye matatizo mengi zaidi,”alisema Mtaka.