Na Erick Kamugisha-DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es salaam umesema jarada la kesi inayowakabili wanakwaya wa Kanisa la Sabato, Kinondoni (SDA) dhidi ya uongozi wa kanisa hilo, limepelekwa kwa hakimu mfawidhi kwa ajili ya kupanga hakimu wa kutoa usuluhisho.
Hakimu Esther Mwakalinga alitoa uamuzi wa kufunga jarada na kupelekwa kwa hakimu mfawidhi, wakati kesi hiyo itapokuja kwa kutajwa tena tarehe husika.
“Jarada la kesi hili,litapelekwa kwa hakimu mfawidhi kwa ajili ya kuteua hakimu mwingine wa kuendesha kesi hii na kutoa suluhisho Desemba 27, mwaka huu”,alisema Hakimu Mwakalinga.
Katika kesi ya msingi, wanakwaya wa Kanisa la Sabato, Barnas Katikiro na David Maiba wameishtaki bodi ya wadhamini na Mchungaji wa Kanisa hilo, Masunya Antory na Joseph Mgwabi.
Wanakwaya hao, walilalamika kwa uongozi wa kanisa hilo wamewatumia waimbaji wengine kufanya mkanda wa video ,wakati watu hao hawakuingiza sauti katika mkanda huo.
Pia wanalalamikia kuwapo mkanganyiko wa Katiba ya kwaya na kudai mahakama ina mamlaka ya kudhibitisha kuwapo jambo hilo.
Kutokana na malalamiko hayo, walifungua kesi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni dhidi ya viongozi wa kanisa hilo, hata hivyo viongozi hao waliweka pingamizi lenye hoja tatu zilizotaka kesi itupuliwe mbali.
Novemba 27, mwaka huu pingamizi hilo lilisikilizwa na mahakama na kulitupiliwa mbali na kupanga kesi hiyo kusikilizwa na kutoa usuluhisho Desemba 27, mwaka huu.