26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

KESI YA VIGOGO CHADEMA KUANZA KUUNGURUMA JULAI 31

                                                                |Kulwa Mzee, Dar es Salaam


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru viongozi tisa wa Chama cha Demekrasia na Maendeleo (Chadema) katika kesi inayowakabili viongozi hao akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe kusomewa maelezo ya awali Julai 31, mwaka huu na mashahidi kuanza kutoa ushahidi.

Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri ametoa uamuzi huo leo Jumatano Julai 25, baada ya kufahamishwa kwamba maombi yaliyowasilishwa Mahakama Kuu na viongozi hao yalitupwa kwa sababu yalikosa vigezo vya kisheria na pia iliona maombi hayo yalikuwa ni batili.

Kutokana na hatua hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ameiomba mahakama kuipangia kesi hiyo tarehe ya usikilizwaji wa awali na baada ya hapo zipangwe tarehe mfululizo za kuanza kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Wakili wa upande wa utetezi Nashon Nkungu kwa niaba ya Wakili Peter Kibatala na Jeremiah aliomba kesi iahirishwe kwa muda mrefu lakini Wakili Nchimbi alipinga akidai  hoja hizo hazijawekwa katika kumbukumbu za mahakama aliomba kesi ipangiwe tarehe ya usikilizwaji wa awali  na tarehe za kesi kusikilizwa mfululizo kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliipanga kesi hiyo kwa ajili ya usikilizwaji wa awali  Julai 31,mwaka huu na kuutaka upande wa utetezi iwapo watakuwa na hoja zozote kuhusiana na maombi yao ya kesi kuahirishwa muda mrefu uwasilishe.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles