29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Kesi ya ole Nangole yakwama

nangoleNa ELIYA MBONEA, ARUSHA

MAJAJI watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, wameahirisha kutoa uamuzi wa rufaa namba 129 ya mwaka 2016 inayopinga kuvuliwa ubunge wa Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema) hadi Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, watakapoingizwa kwenye rufaa hiyo.

Uamuzi wa rufaa hiyo, ulitolewa jana mjini hapa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, John Kahyoza kwa niaba ya jopo la majaji, Sanda Mjasiri, Mussa Kipenka na Profesa Juma Ibrahim.

Akisoma uamuzi huo, Msajili Kahyoza alisema baada ya Mahakama ya Rufaa kupitia sababu sita zilizowasilishwa na Wakili Kimomogolo kwa niaba ya mkata rufaa ambaye ni ole Nangole, mahakama ilizitaka pande hizo kutoa hoja za kupinga au kutetea rufaa.

Alisema kwamba, mahakama imeamua kuchukua uamuzi huo kwa kuwa awali wakili, Dk. Masumbuko Lamwai anayemwakilisha mjibu rufaa ambaye ni Dk. Kiruswa aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo hilo, kuwasilisha pingamizi akiliomba jopo la majaji kuitupa rufaa hiyo kwa kile alichodai ilifunguliwa kimakosa.

Akielezea baadhi ya hoja, Msajili Kahyoza alisema katika utetezi wake, Dk. Lamwai alidai rufaa hiyo ilifunguliwa bila Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Msimamizi wa Uchaguzi, kutajwa.

Baada ya hoja hizo, alidai Wakili Kimomogolo alidai pingamizi hilo halikuwa na msingi kwa kuwa mkata rufaa hakuwasilisha taarifa, nyaraka na sababu za kukata rufaa kwa wahusika wote wawili.

“Baada ya jopo la majaji kupitia hoja hizo, lilibaini kuwapo kwa kasoro na endapo uamuzi wa rufaa ungetolewa bila kuwasikiliza mwanasheria mkuu wa Serikali na msimamizi wa uchaguzi, mahakama hiyo ingekuwa imewatia hatiani bila kuwasikiliza.

“Mahakama imelazimika kutumia mamlaka yake, kwamba katika mazingira ya kesi hii ya uchaguzi uliotenguliwa kwa kuzingatia au kushindwa kuzingatia vifungu na taratibu za uchaguzi, mkata rufaa alitakiwa kuwaweka katika rufaa yake watu hao wawili.

“Kama hilo lingezingatiwa, mahakama ingekuwa imetoa haki ya kikatiba ya wao kusikilizwa mbali na kupewa tu taarifa kama ilivyoelezwa.

“Kwa hiyo, mahakama imelazimika kutoa kibali kwa mkata rufaa (Ole Nangole), kurekebisha taarifa zake na kisha awaunganishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi katika rufaa yake.

“Lakini pia Mahakama ya Rufaa imeagiza nyaraka zitakazorekebishwa ziwe zimekamilika ndani ya siku 21 tangu uamuzi huo ulipotolewa,” alisema Msajili Kahyoza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles