KESI YA MBOWE, DC YAANZA KUSIKILIZWA

0
755

Na UPENDO MOSHA – MOSHI


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi, jana ilianza kusikiliza kesi inayomkabili Mkuu wa Wilaya (DC) ya Hai, Gelasius Byakanwa.

Kiongozi huyo amefunguliwa kesi na Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Ltd, inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Katika shauri hilo, kampuni hiyo inamlalamikia mkuu huyo wa wilaya kwa kushiriki kuharibu shamba la mboga mboga linalomilikiwa na Mbowe katika Kijiji cha Nshara wilayani Hai, Mkoa wa Kilimajnaro.

Wakili wa upande wa utetezi anayemwakilisha mkuu huyo wa wilaya, Modestus Njau, aliiomba mahakama hiyo kukubali ombi la

kumjumuisha katika shauri hilo Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutokana na umuhimu wake.

Pamoja na hayo, wakati kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Aishael Sumari ikiendelea, upande huo wa utetezi uliiomba

mahakama hiyo iahirishe shauri hilo ili kupata muda mzuri wa kupitia madai ya mlalamikaji.

Akizungumza mahakamani hapo, wakili huyo alidai kuna umuhimu wa kumjumuisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kesi

hiyo kwa kuwa mshtakiwa ni mkuu wa wilaya na anashtakiwa kutokana na majukumu ya Serikali aliyokuwa akiyatekeleza.

Kwa mujibu wa Wakili Njau, sheria ya Tamisemi ya mwaka 1997, sehemu ya 14, kifungu kidogo cha kwanza na cha pili, kinataja kazi za mkuu wa wilaya na majukumu yake na kwamba majukumu hayo ndiyo yaliyosababisha afikishwe mahakamani.

Kutokana na maombi hayo, Wakili wa Kampuni ya Uwakili ya D’Souza & co ya jijini Arusha inayoiwakilisha Kampuni ya Mbowe, Meirad Souza, alikubaliana na maombi hayo, lakini akataka yawasilishwe kwa maandishi.

Akitoa uamuzi wake, Jaji Sumari alimtaka mdaiwa kuleta majibu pinzani ya kiapo, Julai 27 mwaka huu na mlalamikaji arudishe majibu Agosti 3,

mwaka huu.

Pamoja na hayo, Jaji Sumari aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14, mwaka huu itakapoendelea kusikilizwa.

Juni 30 mwaka huu, Kampuni ya Uwakili ya D’ Souza & Co ya jijini Arusha, kwa niaba ya Kampuni ya Kilimanjaro Veggies Ltd,

inayomilikiwa na Mbowe, ilimfungulia kesi mkuu huyo wa Wilaya ya Hai na kumtaka alipe fidia ya zaidi ya Sh milioni 549.3.

Katika kesi hiyo namba 20/2017 yenye maombi madogo namba 51/2017, mdai anaomba zuio la muda liweze kutolewa dhidi ya mkuu huyo wa wilaya ili asifanye chochote katika shamba lililoharibiwa mazao lenye ukubwa wa ekari 2.7.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here