JAJI wa Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha, Lameck Mlacha, anatarajia kutoa hukumu juu ya mvutano wa kuuaga mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa Geita marehemu Alphonce Mawazo jijini Mwanza.
Jaji Mlacha anatarajia kutoa hukumu hiyo leo saa saba mchana baada ya pande zote mbili kueleza hoja zao.
Mawakili wa Serikali, Seth Mkemwa na Emilly Kilia ambao wanamtetea Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo aliyezuia mwili wa Mawazo usiagiwe Mwanza, jana waliingia katika mvutano wa kisheria na wanasheria wa Chadema, John Mallya, James Milya na Paul Kipeja wanaomtetea Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa marehemu Mawazo.
Mvutano huo ulihusu ni wapi yalipo makazi na familia ya marehemu Mawazo kwani mawakili wa Serikali walitumia zaidi nyaraka za polisi ambazo marehemu aliwahi kuzitumia wakati wa kujieleza katika vyombo vya dola katika makosa mbalimbali aliyowahi kutuhumiwa nayo.
Pia, mawakili hao waliieleza mahakama hiyo, kwamba sehemu kubwa ya maisha ya marehemu Mawazo, yalikuwa nje ya Mkoa wa Mwanza. Kutokana na hali hiyo, waliiomba mahakama iruhusu heshima za mwisho za Mawazo zitolewe mkoani Geita na si kwingineko.
Pamoja na maelezo hayo, mawakili hao walisema Kamanda Mkumbo hajazuia mwili wa marehemu usiagiwe Mwanza na badala yake walisema walifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutetea agizo la Kamanda Mkumbo la kuzuia shughuli za kuuaga mwili wa marehemu Mawazo zilizotarajiwa kufanyika Novemba 21, mwaka huu jijini Mwanza.
Kutokana na maelezo hayo yaliyoonekana kujichanganya, wasikilizaji wa shauri hilo, waliangua vicheko vya chini chini.
Akiwasilisha hoja kwa Jaji Mlacha, Kilia alisema wao kama watetezi wa Jamhuri katika kesi hiyo namba 11/2015, watajikita kuelezea alipozaliwa marehemu Mawazo hadi Novemba 14, mwaka huu alipokutwa na mauti mkoani Geita ili kuleta uhalisia ni wapi anatakiwa kuagwa.
“Mheshimiwa Jaji, tunatambua umuhimu wa kesi hii, yaani tunataka uamuzi wa haraka ndiyo maana tutajikita kwenye hoja ya alipozaliwa, aliposoma, alipofanya kazi na mauti yalipompata marehemu alikuwa wapi.
“Kwa kifupi, marehemu alizaliwa eneo la Butundwe ambayo ipo Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza.
“Alisoma Shule ya Msingi Chamamba iliyopo Sengerema, alisoma Shule ya Geita kwa wakati huo ilikuwa Mwanza kabla ya mkoa kugawanywa, hivi sasa ipo Geita, kidato cha tano na sita alisoma Lusanga-Sikongo mkoani Tabora, aliendelea na masomo ya ualimu katika Chuo cha Butimba hapa Mwanza.