Kesi ya Lissu kusomwa leo Mahakama Kuu

0
560
Tundu Lissu

Anna Potinus

Kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ya kupinga uamuzi wa kuvuliwa kwake ubunge kutokana na kutohudhuria vikao vya bunge kwa karibu miaka miwili inasomwa leo Alhamisi Agosti 15, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Akizungumzia na chombo kimoja cha habari akiwa nchini Ubelgiji kuhusu uwepo wake mahakamani Lissu amesema anayetakiwa kufika mahakamani ni mtu mwenye mamlaka ya kisheria aliyompatia yeye mwenyewe.

Lissu alifungua kesi mahakamani chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka kisheria kufanya hivyo.

“Kesi inapopangiwa siku ya kusikilizwa au kutajwa au kwa hatua nyingine za kimahakama, pande zote huitwa mahakamani ni nyinyi mnaovutana au wawakilishi wenu wa kisheria au mawakili wenu,” amesema.

“Mimi nimefungua kesi kwa kutumia mwakilishi wa kisheria, mtu ambaye nimempa mamlaka kwa maandishi ili kufungua kesi yangu na kuiendesha kwa niaba yangu,” amesema.

Amesema kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu Septemba 7 mwaka juzi na kwamba Bunge lilikuwa na wajibu wa kujua kuhusu maendeleo ya afya yake.

Lissu amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za bunge la Tanzania, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu mbunge anayeumwa sio wajibu wa mbunge mwenyewe bali ni wajibu wa madaktari walioajiriwa na bunge.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here