25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya Kitilya ngoma mbichi

KitilyaNa Veronica Romwald, Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuandaa maamuzi ya kuondoa shtaka la nane la utakatishaji fedha linalomkabili Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya.

Kitilya anakabiliwa na shtaka hilo pamoja na waliokuwa wafanyakazi wa Benki ya Stanbic Tanzania, Sioi Sumari na Shose Sinare, wanaotuhumiwa kughushi na kutakatisha Dola milioni sita.

Washtakiwa hao waliiomba mahakama kuwaondolea shtaka la nane linalowazuia kupata dhamana.

Kesi hiyo iliitwa mahakamani jana kwa ajili ya kutolewa uamuzi wa kuondolewa kwa shtaka hilo lakini Hakimu Emilius Mchauru alisema ameshindwa kuandaa uamuzi kwa sababu ya mwingiliano wa kimajukumu.

Washtakiwa hao Kitilya, Shose na Sioi, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka huu wakikabiliwa na mashtaka nane likiwamo la utakatishaji wa Dola milioni sita za Marekani ambazo ni sawa na zaidi ya Sh bilioni 12.

Mashtaka yao yanatokana na tuhuma za ufisadi ulioipotezea Serikali zaidi ya Sh trilioni 1.3 katika kipindi cha kati ya mwaka 2012 na 2013 za uuzaji wa hati fungani.

Wakati huo huo, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi imetupilia mbali ombi la Diwani wa Kata ya Segerea, Patrick Assenga na wenzake wanane la kutaka kufungua shauri la kuwawakilisha wakazi 2,619 waliowekewa nyumba zao alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.

Katika kesi yao ya msingi, wananchi hao wanaiomba mahakama kuzuia amri ya Serikali ya kubomoa nyumba zao ambazo zinadaiwa kuwa eneo la Bonde la Msimbazi.

Akizungumza mahakamani hapo jana, Jaji Fredrika Mgaya, alidai ombi hilo lilikuwa halijakidhi matakwa ya kisheria.

“Mmesema mnaomba kuwawakilisha wakazi 2,619 lakini hamjaleta karatasi ambayo watu hao wameisaini kuonyesha makubaliano yenu, tuliyonayo huku mahakamani ni ile ya Manispaa ya Ilala ambayo inaonyesha wakazi wanaopaswa kubomolewa nyumba zao. Hivyo mnapaswa kuyaleta majina hayo kwa mujibu wa sheria,” alidai.

Aidha, Jaji Mgaya alidai kwa kuwa ombi hilo la kwanza limeshindwa kukidhi matakwa ya kisheria na ombi lao la pili la kuitaka mahakama izuie Serikali kubomoa nyumba zao, limetupiliwa mbali.

“Lakini kimsingi mahakama haiwezi kuizuia Serikali kwa sababu kuna hoja za msingi isipokuwa tunaiomba itumie muda wa miezi minne kibinadamu kuja kuzungumza nanyi kuwaelimisha kwanini mnapaswa kuhama mabondeni na hii ni kwa ajili ya maisha na afya zenu,” alidai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles