27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kina Mbowe yakwama kusikilizwa

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Dar es Salaam, imekwama kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwa sababu Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amefiwa na kaka yake.

Kesi hiyo ilitakiwa kuendelea kusikilizwa jana pamoja na kutolewa uamuzi kuhusu mabishano ya kuangalia picha za video zinazodaiwa kuonyesha wafuasi na washtakiwa wakiandamana.

Wakili Peter Kibatala akiwakilisha washtakiwa, alidai kuwa aliandika barua mahakamani akiomba ruhusa kwa washtakiwa wawili, Mbowe na Heche, kwamba wamefiwa na kaka zao kwa nyakati tofauti, hivyo wanaweza kukwama kufika mahakamani.

“Mheshimiwa tuliandika barua tukidhani wote wangeshindwa kufika mahakamani, lakini kwa bahati mheshimiwa Mbowe ameweza kufika isipokuwa Heche ndio wanazika leo (jana), tunaomba kuahirisha kesi hadi tarehe nyingine,” alidai.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akijibu alidai hana neno la kuongeza katika maombi hayo, isipokuwa alipendekeza kesi ipangwe kwa tarehe za karibu ili shahidi wa sita amalize ushahidi wake.

“Mheshimiwa, shahidi tunamshikilia kwa wiki mbili sasa, anatakiwa kwenda Nairobi kwenye mafunzo, wenzake wameshaenda, tunaomba tarehe ya karibu na mfululizo ili amalize aweze kusafiri,” alidai Nchimbi.

Hakimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuamuru isikilizwe mfululizo kuanzia Agosti 15, 16, 19, 21 na 22.

Mara ya mwisho kesi hiyo kufika mahakamani, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi, aliomba mahakama iangalie picha za video katika kielelezo namba nne na tano kilichotolewa na shahidi wa sita, Koplo Charles.

Aliomba mahakama iweke mazingira wezeshi ili kielelezo hicho kiweze kuangaliwa, kwani ni sawa na kielelezo cha nyaraka, kikitolewa lazima kisomwe.

Akijibu, Wakili Kibatala alidai jukumu la kuweka mazingira wezeshi ni la upande wa Jamhuri ambao wangeweza kufanya mambo mawili.

Alidai kwanza wangeandaa mazingira, wangetoa waya unaotumika kwenda kwenye screen kuwezesha picha kuonekana kama kielelezo mahakamani ili wakitumie na pili wangeweza kuwasiliana na uongozi wakaomba ukumbi wa video uliopo watumie kwa kuihamishia mahakama huko.

Wakili Kadushi akijibu, alisema hoja zote mbili hazina mashiko, hazikidhi kuitwa pingamizi katika macho ya kisheria na hazikidhi vigezo.

Alidai hoja za Kibatala ni maoni yake, sio kila kitu kinaweza kutolewa mahakamani kama kielelezo.

“Hayo ni mazingira wezeshi yanayowekwa na mahakama yenyewe na wala si Jamhuri, vifaa hivyo vinatakiwa viwepo mahakamani kama zilivyo mahakama za wenzetu.

“Hilo ni jukumu la mahakama katika kuiwezesha kesi kusikilizwa. Mheshimiwa mahakama yako tukufu inatakiwa kuwezesha kielelezo namba tano kisomeke.

“Tunaomba mahakama iweke mazingira wezeshi ili kielelezo kiangaliwe, kiingie katika kumbukumbu,” alidai Kadushi.

Mbali ya Mbowe na Heche, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu Taifa, Dk. Vicent Mashinji, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu Taifa, Zanzibar, Salum Mwalimu, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani ya kutenda kosa la jinai, ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, Bulaya alishawishi kutenda kosa la jinai katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni, kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwiline na askari polisi wawili; Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles