24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kina Mbowe: Shahidi aeleza alivyopigwa jiwe na kuzimia

NA KULWA MZEE

-DAR ES SALAAM

SHAHIDI wa tatu katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake nane, Koplo Rahim amedai waandamanaji walirusha mawe na jiwe moja lilimpiga shingoni akapoteza fahamu.

Koplo Rahim alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akiongozwa na Wakili wa Serikali, Simon Wankyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thoma Simba.

Alidai wanachama wa Chadema wakiongozwa na viongozi wao waliandamana kutoka viwanja vya buibui kuelekea kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni wakiwa na mawe, chupa za maji na baadhi walivaa mzula hawakuonekana nyuso zao.

Waandamanaji walizuia kuandamana lakini walikaidi ndipo ilipotolewa amri ya kuwapiga mabomu ya machozi ili wasiendelee.

“Moshi wa mabomu ya machozi ulikuwa unarudishwa na upepo upande ambao tulikuwepo askari, moshi ulirudi kwetu, nilipigwa jiwe nikapoteza fahamu, nikipelekwa Polisi Kilwa Road kwa matibabu, nililazwa hapo, nilipopata fahamu nikakumbuka sina silaha, sijui nani alinipiga jiwe.

“Alikuja afande Ndelengi hospitali nikamuuliza kuhusu silaha yangu, akaniambia alichukua mwenzangu iko Oystebay, ilirudishwa ikiwa na silaha zake,” alidai shahidi huyo.

Akihojiwa na Wakili Peter Kibatala, alidai hajui kifungu gani katika kanuni za Polisi (PGO) inayoeleza kuhusu kurejesha silaha.

Alidai silaha inaporejeshwa lazima ikaguliwe na kwamba Polisi akitumia silaha vibaya anachukuliwa hatua za kisheria.

Alipohojiwa kama anafahamu katika maandamano Akwiline Akwilina akifariki dunia, alidai alisikia kama wengine na kwamba hafahamu kama kuna Polisi wawili wanatuhumiwa kwa mauaji hayo.

Shahidi hafahamu kama risasi 90 zilipigwa katika maandamano ya Chadema..

Mbali Mbowe, washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi ni Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari mosi na 16, mwaka 2018, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles