Na MANENO SELANYIKA
-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeahirisha kesi inayomkabili Kamishna wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake hadi Febuari 3, mwaka huu itakapotajwa tena.
Imeelezwa mahakamani hapo jana wakati shauri hilo lilipotajwa kwamba sababu ya kuahirisha kesi hiyo kwa mara nyingine ni upelelezi kuendelea pia Hakimu anayeiendesha, Syprian Mkeha, yupo likizo.
Kesi hiyo imeahirishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage, huku upande wa Serikali ukisimamiwa na Wakili Mutalemwa Kishenyi, wakati ule wa utetezi ukiongozwa na jopo la mawakili watatu wakiongozwa na Masumbuko Lamwai.
Mbali ya Kitilya, washtakiwa wengine ni Miss Tanzania mwaka 1996, Shose Sinare na aliyekuwa Mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane likiwamo la utakatishaji wa fedha kiasi cha Dola milioni sita za Marekani.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo katika tarehe tofauti kati ya Machi, 2013 na Septemba, mwaka juzi wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola milioni 550 za Marekani kwa Serikali ya Tanzania kutoka Benki ya Standard ya Uingereza.
Hata hivyo, Aprili 27, mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia shtaka hilo baada ya upande wa utetezi kuiomba mahakama iliondoe shtaka hilo kwa madai kuwa halijakidhi vigezo vya kisheria kwa kuwa hakuna maelezo ya wazi jinsi walivyotenda kosa hilo.
Upande wa utetezi uliomba Serikali iharakishe upelelezi kwa sababu wateja wao wamekaa mahabusu kwa kipindi kirefu.