NA KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
KAIMU Mkurugenzi Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Grace Sheshue (52), amedai mshtakiwa Bedason Shallanda alikuwa Kamishna wa Sera na mshtakiwa Alfred Misana alikuwa Kamishna Msaidizi wa Madeni, wakati wa mchakato wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 550.
Grace amedai hayo pamoja na kuwasilisha vielelezo vya barua za uteuzi wao ambavyo vilipokewa bila kupingwa.
Shahidi huyo wa tatu wa upande wa Jamhuri, alidai hayo jana Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, alipokuwa akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Hashimu Ngole.
Alidai alianza kukaimu nafasi aliyonayo Machi 13 mwaka jana na kabla ya hapo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Utawala na Rasilimali Watu wa wizara hiyo tangu mwaka 2014.
Grace alidai Idara ya Sera inaongozwa na Kamishna na kati ya mwaka 2011 hadi 2013 Kamishna alikuwa mshtakiwa Bedason Shallanda na Kamishna Msaidizi wa Madeni alikuwa mshtakiwa Alfred Misana.
“Barua ya uteuzi kutoka Wizara ya Fedha ilisema, kuhusu kuteuliwa na kupandishwa cheo kwa Bedason Shallanda kuwa Kamishna wa Sera… awali alikuwa Kamishna Msaidizi wa Sera.
“Barua hiyo ya uteuzi ilikuwa ya Oktoba 10 mwaka 2010 yenye kumbukumbu namba PC/23254/95, barua ilieleza uteuzi unaanza Oktoba Mosi mwaka 2010 na mshahara wake ni Sh 2,065,000 bila nyongeza.
“Ilieleza kwamba atakuwa katika majaribu (kipindi cha uangalizi) kwa miezi sita, endapo atashindwa kufanya kazi ataondolewa kwa kibali maalumu,” alidai.
Shahidi alidai katika barua hiyo alielezwa kwamba Serikali itamdhamini mkopo wa gari ndogo kama hana, atapewa nyumba bure bila kulipa kodi, Serikali itamlipia gharama za umeme kwa mwezi Sh 205,000 na gharama ya simu isiyozidi Sh 180,000.
Alidai mshtakiwa alifahamishwa kwamba kazi hiyo aliyopewa ni ngumu na nzito na kama anaikubali athibitishe, barua ikasainiwa na Katibu Mkuu, Ramadhan Kijja.
Akimzungumzia mshtakiwa Alfred, alidai alikuwa Kamishna Msaidizi wa Madeni na barua yake ya uteuzi ya Juni 19 mwaka 2013 yenye kumbukumbu namba CJA.506,067,01,178 na mshahara wake ulikuwa Sh 2,900,000.
Alidai barua ilieleza atakuwa katika majaribu ya miezi sita akishindwa ataondolewa na Serikali itamdhamini gari dogo, atapewa nyumba bure, atalipwa gharama za umeme Sh 205,000 na gharama za simu zisizozidi Sh 180,000.
Grace alidai barua ya Alfred ilisainiwa na Kaimu Katibu Mkuu, Dk. Silvacus Likwelile.
“Mwaka 2016 nilipokea wito kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kuna nyaraka walikuwa wanazihitaji, nilipoangalia zingine zilikuwa zimeshapelekwa, ilibakia nyaraka moja ya muhtasari wa kikao cha 61 cha Kamati ya Wataalamu ya Madeni,” alidai.
Shahidi huyo aliomba kutoa kielelezo cha barua za uteuzi za washtakiwa hao wawili, hazikupingwa na mahakama ilizipokea kama kielelezo namba mbili na tatu.
Hata hivyo shahidi huyo alikwama kutoa kielelezo kingine cha wito kutoka Takukuru baada ya mawakili wa utetezi kupinga huku mawakili wa Jamhuri wakiomba kipokewe.
Jaji Banzi baada kusikiliza hoja zote aliahirisha kesi hadi leo kwa ajili ya uamuzi wa kupokea ama kutopokea kielelezo hicho.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba nne ya mwaka 2019 ni mshindi wa Mashindano ya Urembo (Miss Tanzania) mwaka 1996, Shose Sinare na Sioi Solomon, ambao walikuwa maafisa wa Benki ya Stanbic.
Wengine ni maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, ambaye kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu na Alfred Misana, ambaye kwa sasa yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola za Marekani milioni sita, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.