KULWA MZEE-DAR ES SALAAM
MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imekubali kupokea nyaraka za mkopo wa dola za Marekani milioni 600 katika kesi inayomkabili Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake, ambazo juzi zilizua utata na mawakili wa utetezi kutaka zisipokewe huku wa Jamhuri wakitaka zipokewe.
Nyaraka hizo zilizopokewa na mahakama kama kielelezo baada ya kukubali maombi ya Jamhuri, ni muhtasari wa Kamati ya Taifa ya Madeni wa kumshauri Waziri wa Fedha na Mipango kukopa kiasi hicho.
Mahakama hiyo ilikubali kupokea kielelezo hicho jana mbele ya Jaji Immaculata Banzi baada ya kupitia hoja za pande zote mbili na kukubaliana na hoja za upande wa mashtaka.
Shahidi wa saba wa Jamhuri alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Deodatha Makani aliyetoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Oswald Tibabyekomya.
Katika ushahidi wake, alidai akiwa katika wizara hiyo kabla hajahamia Wizara ya Afya, miongoni mwa majukumu yake ilikuwa kumsaidia Katibu Mkuu kusimamia masijala ambako kunaingia majalada mbalimbali yakiwemo ya madeni na kusimamia matumizi bora ya mali za Serikali.
“Novemba mwaka 2015 nililetewa jalada na Katibu Mkuu likiwa na hati ya kuyaita majalada mbalimbali yaende Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, nilielekezwa kuwasimamia watu wa masijala wahakikishe majalada hayo yanapatikana.
“Takukuru walitaka nyaraka zote zilizokuwa zinahusiana na mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 ambao Standard Bank uliikopesha Serikali ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2012/2013.
“Miongoni mwa nyaraka zilizotakiwa Takukuru ni majalada halisi ya muhtasari wa kikao cha Kamati ya Taifa ya Madeni kikichomshauri Waziri wa Fedha kuhusiana na mkopo huo na makubaliano ya msingi kati ya Stanbic Bank na Standard Bank kwa ajili ya kutoa mkopo huo wa Dola milioni 600.
“Nyaraka nyingine ambayo Takukuru waliitaka, lakini haikuwepo katika orodha ya nyaraka zilizokwenda, ni muhtasari wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Waziri wa Fedha na Stanbic Bank na Standard Bank zilizokuwa zinashughulikia mkopo huo,” alidai.
Shahidi aliomba kutoa nyaraka hizo kama kielelezo mahakamani, lakini maombi hayo yalipingwa na upande wa utetezi huku wakiomba mahakama isipokee.
Wakili Majura Magafu alidai; “Takukuru waliomba wapelekewe majalada halisi, lakini mahakamani hayo majalada hayakuletwa, kilicholetwa ni nyaraka zilizochomolewa mwenye majalada”.
Magafu alidai nyaraka zinakosa uhalali wa kutumika kama kielelezo, shahidi anakosa sifa ya kutoa kielelezo hicho sababu alitakiwa kuleta jalada halisi sio nyaraka.
“Mheshimiwa jaji tunaziamini vipi hizo nyaraka wakati jalada halisi halijaletwa, kama ziliokotwa… tunaomba zisipokelewe kwani hazistahili, labda zitolewe kwa utambuzi kisha aje mtu wa Takukuru na majalada halisi azungumzie hizo nyaraka,” alidai Magafu.
Akijibu Wakili wa Serikali Mwandamizi, Awamu Mbagwa, aliomba nyaraka hizo zipokewe kwa sababu hoja za upande wa utetezi hazina mashiko.
Alidai Jamhuri hawaleti kitu chochote tu mahakamani, ushahidi wanaotaka kutoa wao wanaona unafaa katika kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.
“Kama upande wa utetezi wana wasiwasi wasubiri watapata nafasi ya kuhoji na si kuzuia nyaraka kupokelewa kama kielelezo mahakamani,” alidai Awamu na kuomba mahakama ipokee kielelezo hicho.
Mahakama jana ilikubaliana na hoja za Jamhuri na kuruhusu kielelezo kutolewa kwani shahidi anastahili kutoa sababu ndiye alikuwa mtunzaji.
Baada ya uamuzi huo, mahakama iliahirisha shauri hilo hadi tarehe ambayo msajili wa mahakama hiyo atakapopanga.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba nne ya mwaka 2019 ni mshindi wa Shindano la Urembo Tanzania (Miss Tanzania) mwaka 1996, Shose Mori Sinare na Sioi Graham Solomon, ambao walikuwa maofisa wa Benki ya Stanbic.
Wengine ni maofisa wawili wa zamani wa Wizara ya Fedha, Bedason Shallanda, ambaye kwa sasa yuko Ofisi ya Waziri Mkuu na Alfred Misana, ambaye kwa sasa yuko Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 58, yakiwemo ya kuisababishia Serikali hasara ya kiasi cha Dola za Marekani milioni sita, kujipatia fedha kiasi hicho kwa njia za udanganyifu na utakatishaji fedha kiasi hicho, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuongoza uhalifu na kumdanganya mwajiri.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Februari 2012 na Juni 2015 katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na nje ya nchi wakati wa mchakato kuiwezesha Serikali kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 550 kutoka Benki ya Standard ya nchini Uingereza.