22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

KESI YA KAMANDA BARLOW: SHAHIDI AELEZA MTUHUMIWA ALIVYOANDIKA JINA LAKE AKIWA HAJUI KUSOMA

Na MASYENENE DAMIAN -MWANZA


SHAHIDI wa 16 upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, marehemu Liberatus Barlow, inayomkabili Muganyizi Michael Peter na wenzake sita, Vedastus Pius Mwingo aliieleza mahakama namna mtuhumiwa namba sita, Amosi Abdallah alivyosaini na kuandika jina lake kwenye hati ya maelezo ya onyo wakati hajui kusoma wala kuandika.

Pius ambaye ni Ofisa Upelelezi ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mwanza (RCO), alitoa ushahidi wake mahakamani hapo jana akiongozwa na wakili wa Serikali, Robert Kidando mbele ya Jaji wa mahakama hiyo, Sirilius Matupa.

Alidai mtuhumiwa alisema hajui kusoma na kuandika, anachojua ni kuandika jina lake tu ambalo alijifunza kwa marafiki zake waliokuwa wakimwandikia chini yeye anaigilizia (kukopi).

 

Alidai mahakamani hapo, kuwa Oktoba 21, mwaka 2012 alienda kufanya upekuzi kwa mama mmoja aitwaye, Bahati Agustino, maeneo ya Nyanshana wilayani Nyamagana baada ya kupata taarifa za kiitelejensia kuwa inasadikika mama huyo anatumia simu iliyopotea kwenye tukio la mauaji ya Barlow na baadaye alirudi ofisini kwa RCO na ndipo alipokabidhiwa mtuhumiwa, Amosi Abdallah kumchukua maelezo.

Sehemu ya mahojiano ya Wakili Kidando na shahidi ilikuwa hivi.

 

Wakili: Ulipokabidhiwa huyo mtuhumiwa ulikuwa wapi?

Shahidi: Nilikuwa ofisini kwa RCO Wilaya ya Nyamagana jengo la Polisi Mkoa.

Wakili: Baada ya kukabidhiwa nini kiliendelea?

Shahidi: Nilimchukua nikamweka kwenye chumba cha ofisi hapo kwa RCO kwa ajili ya kuandika maelezo yake.

Wakili: Kazi hiyo uliifanyaje?

Shahidi: Nilijitambulisha kwake, kwamba mimi ni detective Staff Sergeant (SSG),Vedastus Pius mwenye namba E8662.

Wakili: Baada ya kujitambulisha nini kilifuata?

Shahidi: Nilimuonya

Wakili; Ulimuonya kuhusu nini?

Shahidi:Kosa analotuhumiwa nalo ni mauaji

Wakili: Ulimuonya namna gani?

Shahidi: nilimuonya kwamba yeye (Abdallah Petro Amosi Ndayi), nakuonya kwamba unatuhumiwa na kosa la mauaji ambalo ni chini ya kifungu cha 196 kanuni ya adhabu, kwamba sikulazimishi kusema jambo lolote kuhusiana na tukio hili, isipokuwa kwa hiari yako wewe mwenyewe na lolote utakalolisema litaandikwa, linaweza kutumika kama ushahidi dhidi yako mahakamani.

Pia nilimfahamisha anayo haki kisheria kumwita jamaa yake yeyote, mwanasheria wake ama ndugu ili washuhudie wakati anatoa maelezo yake.

Wakili: Baada ya kumweleza hayo ulifanya nini?

Shahidi:Alisema ameelewa na tukaandika jibu la onyo.

Wakili:Sasa yeye alikueleza nini baada ya hapo?

Shahidi:Alisema yeye mwenyewe anatosha hahitaji uwapo wa ndugu yeyote kwa sababu anaamini nitamtendea haki.

Wakili: Baada ya kukwambia hayo, ulifanya nini?

Shahidi:Nilimuuliza kama anajua kusoma na kuandika ili aandike maelezo yake yeye mwenyewe, akasema anajua kuandika jina lake tu ambalo alijifunza kwa wenzake waliokuwa wanamuandikia chini yeye akawa anaiga (kukopi).

Wakili:Baada ya hapo nini kilifuata?

Shahidi:Baada ya hapo alianza kueleza mimi nikawa naandika tuhuma za mauaji

Wakili:Hayo mahojiano wewe ulikuwa unafanya nini?

Shahidi:Nilikua naandika yeye anaeleza

Wakili:Baada ya kumwandikia maelezo ulifanya nini?

Shahidi: Nilimsomea maelezo yake akasema yako sahihi kama alivyoeleza na akaweka sahihi yake, jina lake na alama ya dole gumba kila page(ukurasa).

 

Hata hivyo, kielezo hicho namba 24 cha hati ya maelezo ya onyo kilipingwa na mawakili wa utetezi kutolewa mahakamani hapo kama ushahidi kwa maelezo kwamba kinapingana na kifungu cha 57 kifungu kidogo cha nne (b), (c) na (d) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002.

Wakili wa utetezi, Cosmas Tuthuru alisema kwa kuwa mtuhumiwa hajui kusoma na kuandika, ofisa aliyemhoji (recording officer) hakumruhusu wala hakumuuliza kama anapenda kuongeza, kupunguza au kusahihisha chochote katika maelezo yake na kuweka uthibitisho hivyo ofisa huyo alijiandikia tu bila kufuata mtiririko huo kama kinavyoelekeza kifungu hicho  hivyo kuiomba mahakama isiupokee ushahidi huo (Question statement).

 

Wakili wa mtuhumiwa huyo, Maduhu Ngassa alipinga kutolewa kwa maelezo hayo kwasababu yanapingana na kifungu cha 50 na 51 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA) na kwamba maelezo hayo yanapingwa na mtuhumiwa namba sita ambaye ni mteja wake, kwa madai hayakutolewa kwa ridhaa yake hivyo mtuhumiwa anayakana maelezo hayo.

 

Kutokana mvutano huo,Wakili wa Kidando aliiomba mahakama iridhie kuwapo kwa shauri dogo ndani ya shauri hilo (Trial within a trial) ili kupata ufumbuzi wa mapingamizi hayo kwa mujibu wa kifungu cha 27 sura ya sita cha sheria ya ushahidi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

 

Jaji Matupa, aliridhia ombi hilo na shahidi huyo alianza kutoa ushahidi wake upya kwa ajili ya shauri hilo dogo na kuulizwa maswali mbalimbali na mawakili wa upande wa utetezi wakihoji uwezekano wa mtuhumiwa kusaini na kuandika jina lake kwenye maelezo ya onyo, wakati hajui kusoma na kuandika, shauri hilo dogo (pingamizi) litaendelea leo kwa Pius kuendelea kutoa ushahidi wake na baadaye mtuhumiwa, Amosi Abdallah Petro kujitetea. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,220FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles