31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya David Kafulila yaiva

kafulilaNa Editha Karlo, Kigoma

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya  Tabora jana iliendelea kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kwa kuwataka mlalamikaji na mlalamikiwa kuwasilisha vielelezo vya matokeo ya uchaguzi wa ubunge uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.

Kesi hiyo  No. 2 ya kupinga matokeo ya jimbo hilo ipo chini ya Jaji Fedrind Wambari ambaye alizitaka pande zote mbili kuwasilisha nakala halisi za matokeo ya uchaguzi, yaani fomu namba 21B mahakamani kama ushahidi.

Jaji Wambari alisema Jimbo la Kigoma Kusini lilikuwa na jumla ya vituo 382 vya kupigia kura, hivyo kila upande unatakiwa kuwasilisha fomu hizo ili mahakama iweze kulinganisha hayo matokeo kwa kila kituo.

Mawakili wa upande wa mlalamikiwa ambaye ni mbunge, Husna Mwilima (CCM) waliiomba mahakama iwape siku moja ili waweze kuziandaa fomu hizo na kuziwasilisha mahakamani hapo Aprili 6.

Kutokana na maombi hayo, Jaji Wambari alikubali ombi hilo na kukubaliana kwa pamoja kesi hiyo kuahirishwa hadi  Aprili 6 mwaka huu kwa ajili ya kulinganisha matokeo yaliyopo katika fomu namba 21B.

Katika kesi hiyo aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) anawakilishwa na Wakili Profesa Abdallah Safari pamoja na Tundu Lissu wakisaidiwa na Wakili mwenyeji wa Kigoma, Daniel Lumenyera.

Upande wa mlalamikiwa, Hasna anawakilishwa na  Wakili msomi, Kennedy Fungamtama pamoja na mawakili wa serikali wanaomwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo.

Katika  kesi hiyo, Kafulila anaomba mahakama imtangaze yeye kuwa mshindi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi kifungu No 112 (c) kwa hoja kwamba yeye ndiye aliyepata kura nyingi kwa mujibu wa matokeo ya kila kituo kwenye fomu namba 21B  na kwamba msimamizi wa uchaguzi alimtangaza, Husna Mwilima kinyume cha matokeo halisi.

Mrema afuta Kesi

Wakati huo huo Upendo Mosha kutoka Moshi anaripoti kuwa: Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, imetupilia mbali kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika Jimbo la Vunjo  iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Agustino Mrema (TLP) baada ya kuamua kujitoa katika kesi hiyo.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya Wakili wa Mrema, January Nkoboko,  kuwasilisha ombi la kujitoa katika kesi hiyo baada ya  pande mbili za mlalamikaji na mlalamikiwa wa kwanza kufanya makubaliano nje ya mahakama kwa maslahi ya wananchi wa jimbo hilo.

“Ninaitaarifu mahakama kwamba Malalamikaji  katika kesi hii ambaye ni Mrema, na mlalamikiwa wa kwanza ambaye ni  Mbatia wamefikia makubaliano nje ya mahakama  ambayo yapo katika kumbukumbu za mahakama kwa maandishi”alisema.

Kwa mujibu wa Wakili Nkoboko, kesi hiyo ni ya uchaguzi na kwamba lengo kubwa  la mteja wake kuamua kujitoa katika kesi hiyo ni kulinda maslahi mapana ya wananchi  pamoja na kupunguza gharama za serikali katika uendeshaji wa shauri hilo.

Wakili anayemtetea Mbatia,  Mohamed Tibanyendera akisaidiana na  Faygrace Sadala na Younsaviour Msuya, waliunga  mkono ombi la wakili wa mlamikaji na kuiambia mahakama kuwa kila upande ubebe gharama zake.

Wakili Mkuu wa serikali, Mark Mulwambo, akisaidiana na wakili Ellen Rwijage na Grayson Orcado, waliunga mkono hoja hiyo huku wakiiomba mahakama hiyo iridhie mawakili wa upande wa serikali kulipwa sehemu ya gharama walizotumia katika kipindi chote cha kesi hiyo.

“Hoja ya Mrema kuamua kujitoa katika kesi hii tunakubalina  nayo lakini ikiipendeza mahakama mawakili tulipwe sehemu ya gharama tulizotumia katika kipindi chote cha kesi hii tangu ilipoanza Novemba mwaka jana,”alisema.

Akitoa maamuzi Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Lugano Mwandambo, alisema mahakama imeridhia maombi yaliyowasilishwa na wakili wa Mrema na kwamba kesi hiyo imefutwa kwa mujibu wa sheria ambapo hakuna gharama zozote zitakazolipwa zaidi ya gharama walizokubaliana nje ya mahakama.

“Makubaliano haya ni sehemu halali ya amri ya mahakama hivyo nawataka mzingatie yote mliyoafikiana na sasa shauri hili halipo tena mbele ya mahakama hii,” alisema.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Mbatia ambaye ndiye aliyekuwa mlalamikiwa wa kwanza katika kesi hiyo alisema kwamba wamekubaliana na Mrema kufuta kesi hiyo huku Mrema akikubali kusaini hati ya makubalino ikiwa ni pamoja na kuwalipa mawakili sehemu ya gharama ambayo ni Sh milioni 40.

“Tulikuwa na kesi mahakamani ya kupinga matokeo katika Jimbo la Vunjo, iliyofunguliwa na Mrema lakini tumemaliza shauri hili nje ya mahakama ambapo tumewekeana makubalino mengi ikiwemo Mrema kuridhia kulipa sehemu ya gharama za mawakili ambayo ni Sh milioni 40.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles