25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

KESI KUPINGA UMEYA KINONDONI YAFUTWA

NYUNDO

Na Kulwa Mzee- Dar es Salaam

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imefuta kesi ya kupinga matokeo ya umeya wa Manispaa ya Kinondoni kwa sababu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mahakama ilifuta kesi hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, baada ya kukubali pingamizi la awali lililowasilishwa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta, kupitia kwa wakili wake, Baraka Nyambita.

Kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2016, ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea umeya katika manispaa hiyo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mustafa Muro na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya unaibu meya kupitia chama hicho, Jumanne Mbunju.

Mbali na Sitta, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni George Manyama ambaye ni Naibu Meya wa Manispaa hiyo wote kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kinondoni.

Wadai walikuwa wanapinga uhalali wa uchaguzi uliowaweka madarakani Sitta na mwenzake.

Hata hivyo, Sitta na wenzake waliwasilisha pingamizi la awali wakiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo pamoja na mambo mengine wakidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Akitoa uamuzi jana, Mwijage, alisema aliifuta kesi hiyo kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo baada ya kupitia maelezo ya pande zote mbili.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo la awali, Nyambita, alidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo wala kutengua matokeo.

Nyambita ambaye ni Mwanasheria wa Manispaa ya Kinondoni, alidai kuwa viongozi hao wanaweza kuhojiwa na kuondolewa katika nafasi hizo kupitia vikao vya madiwani na si mahakamani.

Katika hoja nyingine, alidai kuwa  walalamikaji wamewahusisha watu ambao hawakupaswa kuwepo katika kesi hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Serikali za Mitaa.

Pia alidai kuwa mdai wa pili ambaye alikuwa mgombea wa nafasi ya unaibu meya, hana madai yoyote katika kesi hiyo kwa sababu ametumia majina mawili tofauti katika uchaguzi na katika kesi iliyofunguliwa mahakamani.

Kutokana na mdai huyo kutambulika kwa majina mawili tofauti, Nyambita, alidai kuwa jambo hilo linasababisha mkanganyiko kwa sababu mahakama na walalamikiwa wanashindwa kumtambua mgombea huyo ni yupi kati ya aliyefungua kesi ama aliyegombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, akijibu hoja hizo, Wakili wa wadai, Peter Kibatala, akisaidiana na Wakili John Mallya, walizipinga hoja hizo za pingamizi la wadaiwa, wakidai kuwa hazina mashiko kwa kuwa mahakama hiyo ina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Kibatala alidai kuwa meya anaweza kupingwa mahakamani kwa mujibu na sheria, isipokuwa akituhumiwa kwa masuala ya rushwa na kashfa nyingine mbalimbali anaweza kuondolewa na vikao vya madiwani.

Wakili Kibatala alifafanua kuwa kinachojadiliwa mahakamani katika kesi hiyo ni uhalali wa uchaguzi, jambo alilosema limekaa kisheria na haliwezi kusubiri hadi viwepo vikao vya madiwani ndiyo vitengue matokeo au nafasi za wadaiwa.

“Kufanya hivyo anavyodai wakili wa wadaiwa, itakuwa ni sawa na kukubaliana na matokeo batili yaliyowapa ushindi wadaiwa,” alisisitiza Kibatala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles