23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi aliyedaiwa kuiba mil saba/- kila dakika yapelekwa Mahakama ya Mafisadi

PATRICIA KIMELEMETA

MASHAHIDI 82 wanatarajia kutoa ushahidi katika kesi ya uhujumu uchumi iliyohamishiwa katika Mahakama ya Mafisadi, inayomkabili mfanyabiashara aliyetajwa kujipatia Sh milioni saba kwa kila dakika moja, Mohamed Yusufali na wenzake wawili.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Arifal Paliwalla na Meneja wa Benki ya I&M tawi la Kariakoo, Sameer Khan, wanaokabiliwa na mashtaka 544 kwa kuisababishia Serikali hasara ya Sh bilioni 24.

Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana ilimaliza hatua ya kuwasomea washtakiwa hao idadi ya mashahidi ambao ni 82 watakaotoa ushahidi katika kesi hiyo pamoja na orodha ya vielelezo.

Mawakili wa Serikali, Pendo Makondo, akisaidiana na Wakili Mwandamizi, Christopher Msigwa na Faraji Nguka, walidai mbele ya Hakimu Mkazi, Augustine Rwizile, kuwa kesi hiyo itakua na vielelezo 319 na itasikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.

Makondo alidai kuwa awali washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka 506 na wakati wa kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo vyake, mashtaka 38 yakiwamo ya utakatishaji wa fedha yaliongezeka na kufikia jumla ya 544.

Baada ya kumaliza kuwasomea maelezo hayo, Hakimu Rwizile, aliwapa nafasi kama wana jambo la kuieleza mahakama hiyo kabla kesi hiyo kuhamishiwa katika Mahakama ya Mafisadi.

Washtakiwa hao walidai kuwa hawana cha kusema na wanasubiri kupelekwa Mahakama ya Mafisadi kwa ajili ya kuanza hatua ya usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hakimu Rwizile alisema washtakiwa wataendelea kusota rumande hadi Msajili wa Mahakama Kuu atakapowapangia tarehe ya kwenda kusomewa mashtaka yao katika Mahakama ya Mafisadi.

Katika kesi hiyo, Yusufali, anatetewa na  Wakili Jamhuri Johnson, akisaidiana na Edwin Swale, wakati Paliwala anatetewa na Wakili Jeremiah Mtobesya, wakati Khan akitetewa na Wakili Emmanuel Msengezi.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na  mashtaka 64 ya utakatishaji fedha, 72 ya kuwasilisha nyaraka za uongo, 264 ya kughushi, kupanga njama ya kukwepa kulipa kodi na kuisababishia Serikali hasara.

Katika shtaka la kwanza, wanadaiwa kuwa kati ya Januari, 2008 na Januari, 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa Yusufali na Paliwalla, walitenda kosa la kula njama ya kukwepa kodi.

Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2008 hadi mwaka 2016 katika Jiji la Dar es Salaam, Yusufali akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Farm Plant Limited iliyosajiliwa kulipa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nia ya kukwepa kodi, aliwasilisha makadirio ya kodi ya uongo kwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hivyo kukwepa kulipa kodi ya Sh 24,303,777,426.

Katika mashtaka ya kuisababishia hasara yanayomkabili mshtakiwa Yusufali na Paliwalla, inadaiwa kuwa kati ya Januari, 2008 na Januari, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kwa TRA, kitendo kilichoisababishia Serikali kupata hasara ya Sh bilioni 24.

Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama ya Mafisadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles