29.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Kenyatta asema hatokubali kufanyakazi na wanaopinga ajenda yake serikalini

 NAIROBI, KENYA 

RAIS Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema hatofanya kazi na watu wanaojaribu kuzuia ajenda yake serikalini. 

Katika mojawapo ya ishara kwamba rais Kenyatta huenda akaanza kuifanyia mabadiliko serikali yake, rais huyo alikiambia chombo cha habari cha Nation kwamba anatafuta viongozi ambao wataunga mkono ajenda yake serikalini. 

“Nataka watu ambao hawatopinga ajenda yangu ambayo niliandaa na kuahidi Wakenya. Nataka watu ambao wataunga mkono ajenda hiyo. Na katika demokrasia, iwapo unahisi hufurahishwi na uongozi wa kiongozi wako basi…” 

Sentensi hiyo ambayo haikukamilika baadhi wanaona ilionekana kumaanisha kwamba iwapo viongozi hao wanaoegemea mrengo wa Naibu wa Rais, William Ruto wako tayari kushirikiana tena na kiongozi huyo, muda wao umeisha ama ni mfupi kwa wao kufanya hivyo. 

Katika mahojiano yaliopeperushwa moja kwa moja na runinga ya NTV nchini Kenya, kiongozi huyo alionekana kumshutumu naibu wake bila ya kutaja jina lake. 

Rais Kenyatta alisema kuna wengi ambao wamekuwa wakiweka mbele malengo yao ya kisiasa badala ya kuzingatia maendeleo. 

‘’Msikubali malengo yenu ya kisiasa siku ya kesho kuzuia kila unachopaswa kufanya leo. Kile unachofanya leo ndio kitakachoamua ni wapi utakuwa kesho’’,alisema kiongozi huyo. 

Kiongozi huyo alikuwa akizungumza kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kamati kuu ya chama tawala cha Jubilee ambapo viongozi wanaoegemea upande wa Naibu wa Rais, William Ruto wanatarajiwa kuondolewa. 

Matamshi yake yanajiri siku chache tu baada ya baadhi ya wandani wa naibu huyo wa rais akiwemo aliyekuwa kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen na aliyekuwa naibu wa spika katika bunge hilo Kindiki Kithure kupoteza nyadhfa zao.

Huku akiwa amesalia na miaka miwili katika muhula wake wa mwisho, Rais Kenyatta anakamilisha uongozi wake na kuna vitu vitatu anavyoviangazia kwa sasa. 

Tangu naibu wa rais William Ruto kuanza kampeni za mapema kugombea urais 2022, changamoto kuu kwa Kenyatta imekuwa iwapo atamaliza muhula wake wa pili kama kiongozi ambaye alifeli kutimiza ahadi zake kwa Wakenya. 

Ili kutekeleza ajenda yake ya masuala manne makuu serikalini, Rais Kenyatta alimtangaza Waziri wa Usalama wa Ndani, Dk. Fred Matiangi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji wa Maendeleo na Mawasiliano katika baraza la mawaziri, hatua inayomzuia Naibu Rais huyo kukagua miradi ya serikali. 

Lakini cha kushangaza ni kwamba uteuzi huo ulimpatia Matiangi uwezo mkubwa wa kusimamia miradi yote ya serikali. 

Kwa miezi kadhaa , naibu huyo hajahudhuria hafla za rais katika Ikulu ya rais na pia amekosa kushirikishwa katika mikutano ya baraza kuu la usalama ambapo yeye ni mwanachama. 

Wakati mmoja Ruto alisikika akisema kwamba kuna njama ya kumzuia kumrithi rais Uhuru Kenyatta na ‘mfumo’. 

Naibu huyo alinukuliwa Machi mwaka huu, akisema kwamba mfumo huo bila kutoa ushahidi ulikuwa unapanga njama dhidi yake. 

‘’Wale walio katika mfumo huo wanajigamba kwamba sitakuwepo hivi karibuni’’, Ruto aliandika katika mtandao wake wa Twitter. 

‘’Na kwasababu mfumo huo hauwezi kumchagua mtu yeyote, unaweza kuua. lakini kuna Mungu aliye juu mbinguni’’, alimaliza. 

Wakati rais Kenyatta alipoanzisha vita dhidi ya ufisadi, Ruto alidaiwa kuwakosoa wachunguzi na kudai kwamba ilikuwa silaha kuwakabili viongozi wanaodaiwa kuwa karibu naye. 

Naibu huyo wa rais na washirika wake walisema kwamba Shirika la uchunguzi wa jinai ambalo lilikuwa linaungwa mkono na rais lilikuwa halina uwezo wa kisheria kuchunguza uhalifu wa kiuchumi na kwamba lilikuwa linafanya siasa. 

Msuguano mwengine kati ya Kenyatta na naibu wake ni ule ushirikiano wake na Raila Odinga Machi 2017 ambao ulisaidia kuondoa hofu baada ya uchaguzi wa urais wa 2017.

 Rais Kenyatta anasema kwamba hatua hiyo ni miongoni mwa ahadi alizowapatia Wakenya. 

Wakati huo , taifa lote lilikuwa limezongwa na hali ya wasiwasi baada ya kiongozi wa upinzani Odinga, kususia uchaguzi wa marudio ulioagizwa na mahakama ya kilele, ambayo ilikuwa imefutilia mbali matokeo ya uchaguzi yaliompatia ushindi Kenyatta. 

Wachanganuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya wanasema, HandShake ya Uhuru Kenyatta na William Ruto imekuwa chanzo cha mvutano kati ya wandani wa Ruto na wale wa Raila, ambao wanadai kwamba ni njama ya Kenyatta kufutilia mbali ahadi yake ya kumuunga mkono Ruto atakayewania urais kupitia chama cha Jubilee 2022. 

Wanasema kuwa ,rais Kenyatta anategemea handshake na mradi wa BBI uliozinduliwa mwezi Novemba 2019 kama mojawapo ya mipango ya chama tawala cha Jubilee kuunganisha taifa na kumaliza ghasia ambazo zimekuwa zikitokea kila baada ya uchaguzi. 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,609FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles