KENYATTA APUUZA MADAI YA RAILA

0
459

NAIROBI, KENYA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuzilia mbali madai ya kiongozi wa Cord, Raila Odinga, kwamba Serikali inaendesha njama ya kuwasajili wageni kuwa wapigakura.

Aidha alisema Raila ni mwongo kwa kudai maofisa wa Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) ndio wanaotumika katika njama hizo, zinazoashiria mpango wa mapema wa kuiba kura.

Kwenye taarifa katika vyombo vya habari juzi, Rais Kenyatta alisema madai kama haya yanaashiria kuwa viongozi wa upinzani wamebaini kuwa watashindwa.

“Wamebaini hawashindi, ndiyo maana wameanza kuwachochea wafuasi wao mapema wapinge matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti 2017.

“Wale wanaosajiliwa katika shughuli hii inayoendeshwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ni Wakenya. Wale wanaodai kuwa tunawasajili Waganda au raia wa Ethiopia wamekosa vigezo na ya kuwaambia watu.

“Sasa anadai kuwa maofisa wa NIS wanatumika kupanga wizi wa kura. Aidha, anadai kampeni yangu ya kuwahamasisha Wakenya wajiandikishe kuwa wapigakura ni njia nyingine ya kuiba kura. Matamshi hayo yatamwezesha vipi kuvutia kura?” alisema na kuhoji Rais Kenyatta.

Rais Kenyatta alimshauri Raila kuzunguka kote nchini kuomba kura.

Akihutubia wakati wa mikutano ya kuwahamasisha wafuasi wake kujiandikisha kuwa wapigakura katika maeneo ya Pwani, Raila alidai kuwa maofisa wa NIS wamepeleka mitambo ya BVR katika mataifa jirani kwa kuandikisha wapigakura.

Madai ya Raila pia yamepuuziliwa mbali na Waziri wa Usalama wa Ndani, Jenerali Mstaafu Joseph Nkaissery na Mbunge maalumu, Johnson Sakaja.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here